Home » » Hapana Haja ya Kuiogopa Historia ya Uhuru wa Tanganyika

Hapana Haja ya Kuiogopa Historia ya Uhuru wa Tanganyika

Written By mahamoud on Thursday, December 26, 2013 | 6:58 AM

Hapana Haja ya Kuiogopa Historia ya Uhuru wa Tanganyika

Mohamed Said
Mzee Yusuf Halimoja karudi tena safari hii anasema katika kichwa cha makala yake, “Sijasema Uhuru Uliletwa na Nyerere” (Jamhuri Januari 31 Februari 6 2012). Katika makala hii wakati mnakasha (majadilano)unanoga yeye katangaza kuwa anajitoa. Waswahili tuna msemo, “ametoa mbukwa.” Juu ya huko kujitoa madam kanitaja katika makala yake sina budi nami kumpa majibu yangu katika yale niyajuayo katika historia ya uhuru wa Tanganyika. Mzee Halimoja labda kwa utu uzima huwa anasema mengi. Mimi sitajibu kila aliloandika ila nitapita mle ambamo nahisi wasomaji watafaidika na kitu kipya ambacho hawakuwa wakikijua kabla ya hapo.

Si kweli kuwa Nyerere aliongoza juhudi za uhuru peke yake. Nyerere kaja Dar es Salaam mwaka 1952 na akapokelewa na rais wa TAA Abdulwahid Sykes na alikuta mambo yako mbali sana.  Kirilo kenda UNO  na kurudi, TAA ishazungumza na Kamati ya Umoja wa Mataifa inayosimamia nchi zilizokuwa chini ya Udhamini na ishapeleka mapendekezo ya katiba kwa Gavana Twining, TAA imeshaunda Kamati ya Siasa na ikapeleka viongozi wake (Abbas Sykes, Japhet Kirilo na Saadan Abdu Kandoro)  kutembea nchi nzima kuzungumza na wananchi kuhusu madhila ya  ukoloni. Juu ya hayo yote TAA imeshafanya uhusiano na  vyama vingine vya siasa kama African National Congress (ANC) ya Northern Rhodesia chini ya Kenneth Kaunda. (Ally Sykes hadi leo ana barua kadhaa alizokuwa akiandikiana na Kaunda kabla Kaunda hata hajauana na Nyerere). Vilevile Abdulwahid alikuwa kafanya mkutano na Kenyatta wakati wala Kenyatta hajasikia jina la Nyerere. Nia ya mikutano hii ilikuwa kuunganisha juhudi za TAA na KAU katika kupambana na Waingereza.

Kwa wengi mambo haya ni mageni katika masikio yao wameleweshwa na propaganda za TAA hakikuwa chama cha siasa. Simlaumu Mzee Halimoja naamini kabisa kuwa yeye haya hakuwa anayajua. Kwa Mzee Halimoja siasa Tanganyika haikuwezekana bila Nyerere na TANU chama ambacho Nyerere mwenyewe wala hana chimbuko nacho. Halimoja anazungumza kuhusu ujasiri wa Nyerere. Sawa hapana neno lakini je anaujua ujasiri wa Schneider Abdillahi Plantan katika TAA kiasi ambacho Waingereza walimkamata na kumweka kuzuizini? Je Halimoja anajua kisa cha Dome Okochi Budohi Mkenya kadi yake ya TANU na 6 kazi aliyokuwa akifanya katika harakati za TAA kabla hawajaunda TANU akiwa ndiye kiunganisho kati ya TAA na KAU ya Kenyatta? Ninaweza kumpa mifano kocho. Budohi alikamatwa mwaka 1955 pamoja na wanaharakati wengine wa Kenya kwa tuhuma za kuwa Mau Mau. Budohi alifungwa kisiwa cha Lamu kuazia 1955 hadi 1963 Kenya ilipokuwa inakaribia kupata uhuru ndipo alipoachiwa. Budohi akifahamiana vyema kabisa na wazee wangu na nimejifunza mengi kutoka kwake kuhusu TAA na TANU. Lakini kama Mzee Halimoja anataka kubaki na historia ya Nyerere inayoanza na TANU 1954 na kupuuza michango ya wengine mimi sina ugomvi na hilo. Naamini kwa haya machache msomaji kapata yale ambayo hakuwa anayajua kabla na keshatambua kuwa TAA kilikuwa chama cha siasa hata kabla Nyerere hajakutana na Abdu Sykes Dar es Salaam mwaka 1952.

Mzee Halimoja kazungumzia kuhusu Abdulwahid Sykes kuwa kwa nini natumia rejea zake. Napenda kumafahamisha kitu kimoja. Historia ya Nyerere na TANU itakuwa salama na ikafahamika kama inavyofahamika katika historia rasmi mfano wa hii ya Mzee Halimoja ikiwa tu Abdulwahid Sykes utamtoa katika historia ya TAA na TANU na historia ya Nyerere mwenyewe. Lakini pale tu utamkapomleta marehemu Abdu katika historia ya TAA na TANU itakubidi uachane na Nyerere kwanza na urudi robo karne nyuma kupata mwanzo wa harakati na hapo ndipo unapambana na Nyaraka za Sykes na hazitakuwa za Abdulwahid bali za baba yake. Hapo ndipo utakapojua umuhimu wa nyaraka hizi. Kueleza yaliyomo humo katika nyaraka hizo inataka mada itakayojitegemea yenyewe kwani ni historia inayorudi nyuma karne moja. John Iliffe aliondoka na baadhi ya nyaraka hizi ambazo alikabidhiwa na binti yake Abdu Sykes, Daisy Aisha wakati Daisy alipokuwa mwanafunzi wake wa historia miaka ya 1960 katikati Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Iliffe hajazirejesha hadi leo. Nyaraka hizo ndizo zilizomsaidia Illife kuandika historia ya TAA. Kwa nini historia ya harakati ipatikane kwa mtu mmoja tu Abdu Sykes kama anavyouliza Mzee Halimoja, jibu lake ni hili, baba yake Abdu Kleist Sykes ndiye aliyeasisi harakati za siasa Tanganyika mwaka 1929 na ameacha nyuma hazina kubwa ya maandiko. Anaetaka kujua zaidi na asome “Kleist Sykes, The Townsman” na Daisy Sykes katika “Modern Tanzania,” kitabu kilichohaririwa na John Illife.

Mzee Halimoja anasema Nyerere ndiye aliyeandika katiba ya TANU. Nataka nimweke sawa Mzee Halimoja kuhusu katiba ya TANU. Katiba ya TANU haikuandikwa na yeyote yule. Kwa ufupi ni kuwa Nyerere hakuandika katiba ya TANU. TAA Political Sub Committee ilinakili katiba ya Convention Peoples Party (CPP) ya Kwame Nkrumah neno kwa neno. Mzee Halimoja akitaka ushahidi aitafute katiba ya CPP na aifananishe na katiba ya TANU. Hilo la kwanza. Kitu cha pili napenda kumsahihisha kwa heshima zote Mzee Halimoja kuwa hiyo ilani namba 14 aliyoeleza kuwa ilitolewa na Waingereza haikuwa namba 14 bali namba tano ikijulikana kama Government Circular No. 5 (1 August 1953) ikiwakumbusha viongozi wa TAA kutojiingiza katika siasa. Haya yalitokea baada ya serikali kuwa na ushahidi kuwa TAA ilikuwa inafanya siasa dhahir shahir jambo ambalo Mzee Halimoja hataki kulisikia sharti siasa iwe na Nyerere yumo. Baada ya kuona akina Abdu Sykes na Hamza Mwapachu hawasikii wameshikilia tu kuwasakama Waingereza na serikali yao ikatoka Government Circular No.6. Hapa kuna kisa cha kuhadithia lakini kwa makala hii tutajitoa nje ya maudhui. Kipindi hiki wengi walikikimbia chama wakabaki wanamji. Abdulwahid ilibaki kidogo apoteze kazi yake kama Market Master Soko la Kariakoo. Hii ndiyo historia ya siasa ya TAA na TANU niijuayo mie, historia ambayo wazee wangu walikuwa wachezaji wa kikosi cha kwanza na wakinihadithia siku zote hadi walipotangulia mbele ya haki. Jambo la tatu Mzee Halimoja hasemi kweli kuhusu historia ya TANU katika sehemu zile ambazo kanisa lilikuwa na nguvu. Ukweli ni kuwa waliochelewa kuingia TANU si Warufiji na Wangindo bali watu wa Masasi, Peramiho na kwengineko kutokana na shinikizo la Kanisa. Niruhusu msomaji mpenzi nikudokolee kidogo mambo kutoka katika hazina ya wazee wangu.

Mkutano wa kwanza wa TANU 1955 ulihudhuriwa na Salum Mpunga na Ali Ibrahim Mnjawale kutoka Lindi. Mkutano huu ulifanyika Dar es Salaam Ukumbi wa Hindu Mandal.  Baada ya mkutano, wakati wajumbe wengine wanaondoka kurudi kwenye majimbo yao, Mpunga na Mnjawale walibakia nyuma kukutana na uongozi wa makao makuu wa Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe, Said Chamwenyewe, Oscar Kambona na wengineo. Mpunga na Mnjawale waliwafahamisha viongozi wa makao makuu kuhusu hali mbaya ya siasa Jimbo la Kusini. Mbali na kampeni za kuipinga TANU za Liwali Yustino Mponda ambae Mzee Halimoja anamfahamu vyema kabisa, katika ziara yake Lindi Gavana Twining aliwatahadharisha Waafriika wa Tanganyika wasijihusishe na “wafanya fujo” wanaotaka kuzusha vurugu. Twining alikuwa akitoa onyo hili akiikusudia TANU. Hotuba hii ya Gavana iliwatisha wananchi wengi kutoka sehemu za kusini kujiunga na TANU.

Mpunga na Mnjawale waliomba Nyerere aende majimbo ya kusini kuhamasisha wananchi ili wakabiliane na fitna za Gavana Twining na kampeni za kupinga TANU zilizokuwa zikiendeshwa na Liwali Yustino Mponda. Ukweli ni kuwa Nyerere hakutaka kwenda katika ziara ile akijua kuwa huko alikuwa anakwenda kupambana na kanisa lake uso kwa macho. Juu hayo yote Mpunga na Mnjawale katika kikao kile walimsisitizia Nyerere umuhimu wa yeye kwenda Lindi ambako kunaweza kuwa ndiyo chanzo cha TANU kupata ufanisi Newala, Songea, Tunduru na Masasi ambako kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya TANU. Katika sehemu hizo Kanisa lilikuwa likiwazuia Wakristo kujiunga na TANU. Sheikh Suleiman Takadir, Said Chamwenye, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe wote waliunga mkono ule ujumbe wa Lindi juu ya suala hili. Baada ya kufikia makubaliano, Mpunga na Mnjawale walipewa barua ya kuthibitisha safari ya Nyerere. Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani walifuatana na Nyerere kwenda Jimbo la Kusini kuondoa wasiwasi na woga uliozushwa na Gavana Twining na kibaraka Yustino Mponda.

Nyerere na msafara wake ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji kidogo nje ya mji. Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda. Mbali na Mpunga na wale wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam mwezi uliopita, hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi. Mpunga, dereva wa lori, alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere apate kumuona. Baada ya Nyerere kumtia Mpunga machoni, Mpunga alimwendea kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha aliligeukia lile kundi la watu kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja jina lake kwa sauti kubwa. Baada ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere. Nyerere na ujumbe wake ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya TANU kwenye nyumba ya Suleiman Masudi Mnonji. Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya seremala mmoja, Issa bin Ali Naliwanda. Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale Nyerere na ujumbe wake, si kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote. Ilichaguliwa na kupewa heshima hii kwa sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo basi ilirahisishia TANU kazi ya ulinzi wa Nyerere. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili na Nyerere aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya ibada.

Kanisa Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya Hindi. Lindi ulikuwa mji wa Waislam. Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye viwanja vya kanisa. Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi katika ofisi za serikali. Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa miaka na Waislam wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani. Hakuna mtu katika uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala mahali popote pale. Uongozi wa TANU wa Waislam mjini Lindi haukumwamini Mkristo yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.

Jumapili hiyo Nyerere aliingia ndani ya kanisa Katoliki mjini Lindi akifuatwa nyuma na walinzi wake Waislam wakiongozwa na Salum Mpunga, dereva wa lori shupavu. Misa hii maalum  ilidumu katika fikra za wale Wakristo waliokuwepo pale kanisani kwa miaka mingi kwa kuwa tukio hilo liliwagusa sana Wakristo walioshuhudia mkasa ule ndani ya kanisa la Lindi. Hii huenda ilikuwa mara ya kwanza na ya mwisho kwa Nyerere kumsalia Mungu wake huku akiwa amesimamiwa na Waislam. DC mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe. Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine wamesimama katika ya jua kali walikuja kumsikiliza Nyerere akihutubia. Ili kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni serikali iliweka askari waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere aliwafikishia watu ule ujumbe wa TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na Waafrika wa Tanganyika lazima wadai uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa imewasili Jimbo la Kusini.

Wasomaji wapenzi katika makala yangu iliyopita nilimpa changamoto Mzee Halimoja aeleze ni akina nani waliingiza TANU kwao huko Masasi na Peramiho. Ukweli ni kuwa hata kugusia hili katika makala yake iliyopita hakuthubutu. Nimempa changamoto aeleze hicho anachokiita “mchango wa pekee wa Nyerere” katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Hilo vilevile limemshinda. Nashukuru kuwa kanijibu ingawa kakwepa baadhi ya mambo muhimu lakini kwa kufanya hivyo kanipa mimi nafasi ya kueleza yale ambayo naamini wengi walikuwa hawayajui. Nyerere hakuwa peke yake katika kuupigania uhuru wa Tanganyika wala hakuandika katiba ya TANU wala harakati za kupigania uhuru hakuzianzisha yeye. Nadhani haya niliyoandika yanatosha kwa sasa na ningependa kumaliza kwa kuuliza swali. Nani leo anawakumbuka wazalendo hawa nilowataja katika makala haya? Je hawastahili watu hawa kuenziwa pamoja na Nyerere?


30 Januari 2012
Share this article :

0 comments:

Post a Comment