MATUNDU KATIKA HISTORIA YA KUPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA
Mohamed Said
Wakati marehemu Abdulwahid Sykes[1]akiwa katika harakati za uongozi wa TAA alikuwa akifanya kazi kama Market Master soko la Kariakoo. Ofisi yake ilikuwa kati ya Mtaa wa Swahili mbele Mtaa wa Mkunguni na nyuma yake Mtaa wa Tandamti. Mtaa huu wa Tandamti umebadilishwa jina sasa unajulikana kama Mshume Kiyate ingawa wahusika hawajabadili kibao sasa takriban miaka kumi na zaidi kwa kuwa wanapinga mabadiliko hayo kwa fikra kuwa kilichopelekea Meya wa Dar es Salaam Kitwana Selemani Kondo kumuenzi Mshume Kiyate ni udini na wala si uzalendo na mchango wa muhusika katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Huenda kizazi cha leo na wanasiasa wa sasa hawawajui mashujaa wa nchi yetu na yaliyokuwa yakipitika pale Kariakoo ofisini kwa Abdulwahid.
Katika ofisi ile alikuwapo Mzee Abdallah yeye alikuwa ndiyo mhudumu wa ofisi na alimjua Mwalimu Nyerere pale ofisini kwa Abdulwahid na anachokumbuka kwa maskhara ni ile kazi yake ya kuchukua kuku pale sokoni akawachinja na kumpelekea Mama Daisy, mke wa Abdulwahid kwa ajili ya chakula cha mchana cha Nyerere na wanaharakati wengine hasa Nyerere alipoacha kazi ya ualimu na kuja kukaa na Abdulwahid kwa muda kabla hajenda Musoma. Pale ndipo ilipokuwa sehemu kuu ya mawasiliano ya TAA. Wakati ule Abdulwahid alikuwa katibu wa TAA na Dr. Vedasto Kyaruzi alikuwa ndiye rais.
Wakati ulikuwa miaka ya mwanzo 1950 na Abdulwahid Sykes alikuwa keshakutana na Jomo Kenyatta Nairobi na kufanya mkutano na KAU nia ikiwa ni kuunganisha nguvu za TAA na KAU yaani juhudi za Watanganyika na Wakenya kupambana na ukoloni. Harakati hizi zilipelekea kuwa na mawasiliano ya karibu sana na ya siri kati ya Abdulwahid Sykes na Kenyatta kiasi kwamba mwaka 1953 Kenyatta alimwalika kwa mara ya pili Abdulwahid Nairobi katika mkutano mwingine ambao alikuwa aende na Dossa Aziz. Ule mkutano wa kwanza Abdulwahid alisindikizwa mkutanoni na Ahmed Rashad Ali ambae baadae alikuja kuwa mtangazaji maarufu wa Radio ya Ukombozi wa Africa (Radio Free Africa) kutoka Cairo . Kutokana na mkutano huu Rashad akaja fahamiana vizuri sana na Kenyatta. Kipindi hiki harakati dhidi ya ukoloni zilikuwa zimepamba moto Afrika.
Kipindi hiki cha miaka ya mwanzo wa 1950 TAA ilikuwa kama vile inatoka usingizini na kuanza kufanya siasa za kweli chini ya uongozi wa vijana baada ya kuuangusha uongozi uliopita uliokuwa umehodhiwa na wazee waliosomeshwa na utawala wa Kijerumani rais wa TAA akiwa Mwalimu Thomas Plantan na katibu wake Clement Mtamila. Abdulwahid na Ally Sykes walikuwa na mawasiliano na Kenneth David Kaunda katibu wa African National Congress pamoja na Asia Socialist Conference Anti-Colonial Bureau. Idara ya Usalama ya kikoloni ikijulikana kama Special Branch walikuwa wakifuatilia kwa karibu sana nyendo za ndugu hawa. Mtafiti akipitia nyaraka za Sykes atakutana na shajara za marehemu Abdulwahid baadhi zikiwa zimeandikwa kwa hati ya kawaida na nyingine zikiwa katika hati mkato. Inaaminika shajara zake za hati mkato ndizo zenye taarifa nyingi za harakati zake za kuanzisha TANU na safari zake nje ya nchi kukutana na wapigania uhuru wengine kama Jomo Kenyatta, Bildad Kaggia, Kung’u Karumba, Achieng Oneko, Fred Kubai na Paul Ngei. Hawa walikuja fahamika kama “Kapenguria Six” kwa kuwa walifungwa jela kwa tuhuma za Mau Mau sehemu hiyo inayojulikana kama Kapenguria.
Bahati mbaya ni kuwa akina Sykes wenyewe hawajaruhusu watafiti kuzisoma shajara za marehemu Abdulwahid ambazo sasa takriban zina umri wa zaidi ya miaka hamsini. Nyaraka za siri za serikali ya kikoloni ambazo sasa ziko wazi huko Uingereza baada ya kupita miaka hamsini zinaonyesha kuwa Abdulwahid wakati akiwa mfanyakazi wa Soko la Kariakoo nyendo zake zilikuwa zikifuatiliwa kwa karibu sana na “Special Branch” kiasi cha kuwa jalada lake la siri limemtaja kama “mtu hatari.” Katika halmashauri ya TAA walikuwapo Waafrika kutoka Kenya na Nyasaland kama Dome Okochi Budohi na Patrick Aoko kutoka Kenya na Denis Phombeah kutoka Nyasaland wakiendesha harakati bega kwa bega na ndugu zao Watanganyika.
Wakati akina Bildad Kaggia na Kenyatta lile kundi la Kapenguria likikamatwa Nairobi baada ya muda Budohi na Aoko nao walitiwa mbaroni Dar es Salaam . Abdulwahid ilibidi akaimu nafasi ya rais baada ya Dr. Kyaruzi kupewa uhamisho kwenda Kingolwira kama adhabu ya kupinga serikali. Kama kuna mtu ana fikra kuwa TAA haikuanzishwa kwa ajili ya kudai uhuru wa Tanganyika basi na aeleze hizi harakati za viongozi wake kuweka mikakati ya pamoja na akina Jomo Kenyatta na Kenneth Kaunda katikati ya 1950 na 1953 na kuweka uhusiano na vyombo kama Asia Socialist Anti- Colonial Bureau ilikuwa ya kutafuta nini. Vilevile aeleze kwa nini serikali ilitoa sekula no. 5 na 6 ikiwaonya Waafrika watumishi wa serikali kuhusu kufanya siasa wakiwa watumishi wa Malkia.
Mwalimu Nyerere na Abdulwahid walikujafahamiana mwaka 1952 na Nyerere alipelekwa nyumbani kwa Abdulwahid na Joseph Kasella Bantu. Nyerere alikuwa akija mjini lazima atapita ofisini kwa Abdulwahid Sykes pale sokoni Kariakoo ikiwa siku za kazi. Siku za Jumapili alikuwa akienda Mtaa wa Mbaruku nyumbani kwa Dossa.
Siku zile akiwa pale kwa Abdulwahid akenda ofisini kwake Kariakoo na wakati wa chakula cha mchana Mwalimu Nyerere alikuwa akiongozana na Shariff Attas ambae alikuwa akifanya kazi chini ya Abdulwahid Sykes kama dalali wa soko. Shariff Attas alikuwa akiongozana na Nyerere kwenda nyumbani kwa Abdulwahid kwa ajili ya chakula. Jambo hili likawafanya Shariff Attas na Mwalimu Nyerere wawe karibu sana na wajuane vizuri. Nyumba ya Abdulwahid Sykes haikuwa mbali sana na soko, ilikuwa Mtaa wa Aggrey na Sikukuu nyumba ya kona. Shariff Attas na Mama Daisy ni mmoja wa watu wa mwanzo kujuana na Mwalimu Nyerere achilia mbali kuwa walikuja kuwa wanachama wa mwanzo wa TANU ilipokuja kuundwa mwaka 1954. Mwalimu Nyerere alipokuja Dar es Salaam na mkewe Mama Maria, Mama Daisy ndiye aliyempokea Mama Maria na kumtoa ukumbi.
Kupitia kwa Abdulwahid Sykes Mwalimu Nyerere akajuana na watu wengine pale sokoni mashuhuri mjini kama Mshume Kiyate, Shariff Mbayamtu na wengineo. Mshume Kiyate akampenda Mwalimu Nyerere kama mwanae. Wakati wa kudai uhuru baina ya 1954 hadi 1961 Mzee Mshume alijitolea kuiangalia na kuitunza familia ya Mwalimu Nyerere ili Nyerere ashughulike na TANU tu asihangaike na adha ya kuhemea chakula cha wanae. Mzee Mshume na Mwalimu Nyerere wote wawili walikuwa wapenzi wa kucheza bao na wakati mwingine Mzee Mshume akicheza bao na Mama Maria. Ofisi ya Abdulwahid pale Kariakoo na ofisi ya Hamza Mwapachu[2]Ilala Wefare Centre ndipo palipokuwa na pilikapilika za ingia toka za wanasiasa wa wakati ule kwa nyakati za mchana na ikiingia usiku harakati zilihamia Tanga Club iliyokuwa Mtaa wa New Street na Mkunguni.
Uchaguzi wa rais wa TAA wa 1953 kati ya Abdulwahid Sykes aliekuwa akitetea kiti chake na Julius Nyerere ulikuwa uchaguzi wa aina yake katika historia ya uhuru wa Tanganyika . Ulitanguliwa na majadiliano ndani ya Kamati Ndogo ya Siasa ya TAA kueleza umuhimu wa kumweka Nyerere katika kiti badala ya Abdulwahid ambae muda wake wa uongozi ulikuwa unakwisha. Hapa ndipo mwanzo wa matundu na chanzo cha matatizo ya historia ya kudai uhuru wa Tanganyika . Kwa kuwa Nyerere mwenyewe hakupata kueleza vipi aliingia TANU inaonekana kama alizuka tu kutoka Musoma akatua Dar es Salaam na kuanzisha TANU. Jambo ambalo haliwezekani.
Ukweli wa mambo ni kuwa uchaguzi baina rais wa TAA, Abdulwahid Julius Nyerere, ulifanyika kwenye Ukumbi wa Arnatouglo tarehe 17 Aprili, 1953. Nje ya uongozi wa TAA ambao ulimpendekeza kugombea nafasi hiyo, Nyerere alikuwa mgeni kabisa kwa wote aliokuwa akiwaomba kura zao. Nyerere alikuwa mgeni na alikuwa hana historia ya kuongoza mapambano ya umma dhidi ya serikali ya kikoloni. Ukoo wa Sykes ulikuwa maarufu na unatambulikana katika siasa za Dar es Salaam kwa takriban robo karne. Ushahidi wa haya unapatikana katika nyaraka kati ya ukoo huu na serikali ya kikoloni. Katika kipindi cha miaka zaidi ya ishirini, serikali kwa nyakati tofauti, kati ya mwaka 1929 hadi 1953 ilikuwa na barua za Kleist Sykes [3] na za mwanaye Abdulwahid wakiwa viongozi wa African Association wakichagiza serikali kuhusu madhila tofauti yaliyokuwa yakiwakabili wananchi. Maarufu katika hayo ni migomo ya wafanyakazi kati ya mwaka wa 1938 hadi 1947 na ule mgogoro wa ardhi ya Wameru.
Uchaguzi ulikuwa kwa kunyoosha mikono. Denis Phombeah[4] aliyekuwa akifanya kazi Ukumbi wa Arnatouglo ndiye alikuwa msimamizi wa uchaguzi. Phombeah aliwaomba Abdulwahid na Nyerere kutoka nje ya ukumbi ili uchaguzi uanze. Wiki nzima kabla ya uchaguzi Phombeah alikuwa akizunguka mji mzima na pikipiki yake akimfanyia kampeni Nyerere. Lakini kwa hakika hakukuwa na haja ya kufanya hivyo. Uongozi wa ndani wa TAA wa Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz na John Rupia ulikuwa tayari umekwishaamua kumpa Nyerere urais wa chama. Uchaguzi ulikuwa kutimiza utaratibu tu. Baada ya Abdulwahid na Nyerere kuombwa na Phombeah kutoka nje, upigaji kura ulianza.
Nyerere alishinda uchaguzi huo dhidi ya Abdulwahid kwa kura chache sana. Huu ulikuwa ndiyo mwanzo wa Nyerere kujulikana katika siasa za Tanganyika. Kuanzia siku ile historia ya Tanganyika ikabadilika na siasa za Tanganyika zikachukua sura nyingine kabisa. Siasa zilichukua sura nyingine kwa sababu walingia watu katika harakati ambao waligeuza mwelekeo kudai haki kwa vipaji vya kuhamasisha watu ambavyo Tanganyika ilikuwa haijapata kuona. Hapa ndipo unapokutana na Titi Mohamed,[5] Tatu bint Mzee, Said Chamwenyewe,[6] Sheikh Suleiman Takadir,[7] na wengine wengi lakini kwa bahati mbaya hawa wote historia imewasahau hawatajwi kabisa.
Nyerere mwenyewe kamwe hajazungumzia kuhusu uchaguzi huu au namna alivyokuja kuongoza TAA Dar es Salaam. Kiasi cha karibu sana alichofika kumhusisha Abdulwahid na historia yake kilikuwa katika ile hotuba ya mwaka wa 1985 ya kuwaaga wazee Dar es Salaam, na kwa bahati mbaya Nyerere alipojaribu kumueleza Abdulwahid, alishindwa kwa kuwa kwa kauli yake alisema hakumbuki cheo alichokuwa akishika Abdulwahid katika TAA wakati yeye Nyerere alipojiunga na chama mwaka 1952. Hata hivyo gazeti la serikali, “Daily News” lilijaribu kurekebisha historia kwa kutaja cheo cha Abdulwahid, ingawa kwa makosa, kwa kusema kuwa Nyerere alipojiunga na TAA makao makuu Abdulwahid alikuwa katibu. Ukweli ni kuwa Nyerere alimkuta Abdulwahid akiwa rais wa TAA. Nini sababu ya mparaganyiko huu?
Kleist Sykes baba yao Abdulwahid, Ally na Abbas ameacha kumbukumbu nyingi zinazoelezea si tu hali ya siasa Tanganyika ilivyokuwa mwanzo wa karne ya ishirini bali zinatoa historia kamili ya mji wa Dar es Salaam na watu wake na jinsi yeye mwenyewe alivyoasisi African Association. Ukipitia nyaraka hizo zinakurudisha miaka mia moja nyuma toka baba yake Kleist, Sykes Mbuwani alipoingia nchini Tanganyika kama mamluki akiwa katika jeshi la Wazulu mia nne wakiongozwa na Mjerumani Von Wissman kuja kupigana na Bushiri bin Salim Pangani na Chifu Mkwawa huko Kalenga. Nyaraka zinaonyesha maisha ya Kleist katika jeshi la Wajerumani katika Vita Kuu ya Kwanza akiwa Aide de Camp (Mpambe) wa Von Lettow Vorbeck. Nyaraka zinafichua vipi Kleist alikuja kuwa mwanasiasa hodari na kiongozi wa chama cha wafanyakazi katika kipindi cha vita kuu mbili za dunia baada ya kukutana na Dr James Kwegyir Aggrey mwaka 1924 na kumshauri aanzishe umoja wa Waafrika katika Tanganyika.
Kutokana na ushauri huu wa Dr Aggrey mwaka wa 1929 Kleist na baadhi ya rafiki zake wa karibu kama Mzee bin Sudi, ambaye wazazi wake walikuwa Wamanyema kutoka Belgian Congo, Ibrahim Hamis - Mnubi ambaye baba yake alitoka Daffur nchini Sudan, Zibe Kidasi, Ali Said Mpima - Mzaramo, Suleiman Majisu, Raikes Kusi, Rawson Watts na Cecil Matola - Myao kutoka Masasi walianzisha African Association, Kleist akiwa katibu muasisi. Gavana wa wakati ule Donald Cameroon akawaonya akina Kleist kuwa wasikiingize chama katika siasa. Mikutano ya mwanzo ya chama hiki ilifanyika Mtaa wa Masasi Mission Quarter Dar es Salaam kwenye nyumba ambayo ilikuja hapo baadae ikanunuliwa na John Rupia. Mwaka wa 1930 katika juhudi za kuikiimarisha chama, Kleist akawa anasimamia ujenzi wa jengo la makao makuu ya African Association, New Street (sasa Mtaa wa Lumumba) ambalo wananchi walikuwa wakijenga ofisi yao hiyo kwa kujitolea nguvu zao wenyewe. Hili ndilo jengo ambalo TANU ilikuja kuzaliwa tarehe 7 Julai, 1954.
Wakristo walionywa na wamisionari wasijihusishe na African Association kwa kuwa harakati zao ni kupinga serikali. Haya yote ameyaeleza Kleist katika kumbukumbu zake alizoacha kabla ya kifo chake mwaka 1949. Abdulwahid akiwa mtoto mdogo alipata kueleza kuwa ameshuhudia kwa macho yake ujenzi wa jengo la TAA kwa kuwa alikuwa akifuatana na baba yake pale New Street siku za Jumapili ambayo ndiyo ilikuwa siku ya ujenzi. Kleist hakuishia hapo baada ya kuasisi African Association mwaka 1929 akaasisi “Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ” (Umoja wa Waislam wa Tanganyika ) mwaka 1933 akiwa katibu. Vyama hivi viwili vikawa vinafanya kazi kwa pamoja kwa kuwa viongozi hao hao wa TAA ndiyo wakajakuwa viongozi wa “Al Jamiatul Islamiyya” na huu ndiyo ulikuwa mtindo hadi mwaka wa 1954 TANU ilipoasisiwa. Mweka Hazina wa “Al Jamiatul Islamiyya” Iddi Faizi Mafongo[8]ndiye aliyekuwa pia mweka hazina wa TANU na “Al Jamiatul Islamiyya” ilitoa fedha katika kuchangia safari ya Nyerere Umoja wa Mataifa mwaka 1955.
Watu wengi hawajui kuwa ile hotuba aliyosoma Nyerere Umoja wa Mataifa iliandikwa mwaka 1950 na Kamati Ndogo ya Siasa ndani ya TAA iliyoasisiwa na Abdulwahid Sykes wajumbe wake wakiwa Sheikh Hassan bin Amir kama mufti wa Tanganyika na Zanzibar ; Dr Vedasto Kyaruzi, Hamza Mwapachu, Said Chaurembo aliyekuwa liwali wa mahakama ya Kariakoo; John Rupia na Stephen Mhando.[9] Kazi ya kamati hii ilikuwa ni kushughulika na masuala yote ya siasa katika Tanganyika. Kuundwa kwake ndiyo hasa ulikuwa mwanzo wa siasa za dhahiri katika Tanganyika na mwanzo wa harakati za kudai uhuru wa Mtanganyika.
Inasikitisha kuwa Mwalimu Nyerere hakupata kueleza chanzo cha hotuba ile ambayo hivi sasa imo katika moja ya vitabu vyake na kwa hakika hiki ni kisa kirefu sana na cha kumvutia mtafiti yeyote. Waraka huu ulokuwa chanzo cha hotuba ya Mwalimu Nyerere Umoja wa Mataifa umepotea na haujulikani ulipo. Jalada lake Tanzania National Archive (TNA) ni tupu na hata “microfilm” ya waraka ule imetoweka. Laiti ungelipatikana mtafiti angeliona sahihi ya marehemu Abdulwahid Sykes, Vedasto Kyaruzi, Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Mwapachu na wajumbe wengine. Mtafiti akitaka kujua vipi African Association iliasisiwa na ni nani wahusika wakuu basi hana budi kusoma nyaraka za Kleist Sykes lakini ikiwa atataka kutafiti kuhusu TANU itabidi asome nyaraka pamoja na shajara za Abdulwahid Sykes.
Ikiwa huu ndiyo ukweli wa historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika huu ubishi wa kuwa nani kaasisi TAA umetoka wapi? Halikadhlika unaweza mtu ukahoji kwa nini waliokuja baada ya TAA waseme kuwa hapa ndipo ilipozaliwa TANU badala ya kusema kuwa hapa ndipo ilipozaliwa TAA? Au vipi ikawa muhali kunasibisha familia ya Kleist Sykes na nguvu ya Watanganyika kujikomboa? Kipi kinachoogopwa? [10] Hivi kweli Nyerere angeweza kuukana ukweli huu mbele ya watu wa kawaida tu na wala si wanasisasa, watu kama Shariff Attas na Mzee Abdallah na akabaki na heshima yake achilia mbali wanasiasa wa wakati ule kama Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Mwapachu, Dr. Kyaruzi na wengineo?
Ama kuenezwa kwa TANU katika majimbo hiyo kazi ilifanywa na wengi ambao leo hawatajwi na hata pale Mwalimu Nyerere alipotoa medali 3979 mwaka wa 1985 katika viwanja vya Ikulu kwa Watanzania waliofanya mengi katika nchi hiii ilistaajabisha wengi kuwa hakuna hata mmoja wa waliopigania uhuru aliyepata heshima hiyo. Si Dossa Aziz, wala Abdulwahid Sykes au Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Yusuf Badi, Tatu bint Mzee, Mshume Kiyate, Mwinjuma Mwinyikambi, Suleiman Masudi Mnonji, Bi. Shariffa Mzee, Sheikh Mohamed Ramia, Zuberi Mtemvu, Ali Mwinyi Tambwe, Hamza Mwapachu, Dr. Kyaruzi, Dr. Michael Lugazia, Ali Migeyo,[11]Suedi Kagasheki, Iddi Faiz Mafongo, Yusuf Olotu, Yusuf Chembera, Salum Mpunga,[12]Hamisi Taratibu, Omari Suleiman,[13]John Rupia, Joseph Kasella Bantu [14]na wengine wengi. Hakuna katika mashujaa wa uhuru aliekumbukwa kwa kupewa medali licha ya kuwa wao walitembea nchi nzima kuieneza TANU pamoja na Nyerere.
Wala si kweli kuwa wazalendo hawa hawakumaliza kazi. Abdulwahid na Ally Sykes walifadhili chama hadi uhuru unapatikana. Inatosha kusema tu Dossa Aziz alifadhili chama hadi kufikia kufilisika kabisa na akafa kijijini Mlandizi akiwa masikini kabisa. Sheikh Hassan bin Amir katika kumbukumbu zake anasema alijiuzulu siasa baada ya uhuru kupatikana na kuanzisha Daawat Islamiyya ili ashughulikie elimu kwa Waislam na hii ndiyo ikawa kisa cha ugomvi baina yake na Nyerere mwishowe Mufti Sheikh Hassan bin Amir akakamatwa kwa amri ya Nyerere na kurejeshwa kwao Zanzibar. Baraza la Wazee wa TANU lilikokuwa na wajumbe 170 wote Waislam chini ya uenyekiti wa Iddi Tulio baada ya kufukuzwa Sheikh Takadir TANU lilishiriki katika mapambano hadi mwisho na lilikuja kuvunjwa na Nyerere mwaka 1963 kwa madai ati wazee wale wa Kiislamu walikuwa wakichanganya dini na siasa. Ama kuhusu Waislam na Nyerere kuhusu udini hili ni somo tosha linalohitaji muda wa pekee. Na ni katika huo udini ndipo iNakapojitokeza leo kwa nini Waislam hawamwiti tena Mwalimu Nyerere Baba wa Taifa bali wanamwita Baba wa Kanisa.
Mwalimu Nyerere alitaka historia ya TANU iandikwe na fikra hii ilitokea katika mjadala ulofanyika kati yake Abdulwahid, Mwalimu Kihere na Dossa Aziz. Mwalimu alimpa kazi hiyo ya uandishi wa historia ya kudai uhuru wa Tanganyika Abdulwahid Nyerere akamteua Dr. Wibert Kleruu awe msaidizi wa Abdulwahid katika kazi ile. Hii ilikuwa baada ya uhuru kupatikana. Historia iliandikwa lakini Nyerere inasemekana alisononeshwa sana na mchango wa familia ya Sykes katika siasa za Tanganyika. Historia ya Sykes Mbuwane na Von Wissman wakati wa enzi wa utawala wa Wajerumani kisha historia ya Kleist Sykes na Von Lettow Vorbeck wakati wa Wajerumani na kuingia utawala wa Waingereza ilikuwa mithili ya mchezo mzuri wa senema kutoka Hollywood. Historia yake binafsi Abdulwahid kuanzia Burma hadi kurejea Tanganyika na harakati zake na akina Kenyatta, Japhet Kirilo [15]na Earl Seaton hadi kufikia Kirilo na Seaton kwenda Umoja wa Mataifa mwaka 1952 iliingiza husda katika moyo wa Nyerere. Husda kama ijulikanavyo ni maradhi yasiyo na tiba.
Historia ile ilimwonyesha baba yake Abdulwahid Mzee Kleist kama Mwafrika alielimika vizuri kwa viwango vya wakati ule. Kleist akizungumza Kijerumani na Kiingereza, akijua kupiga chapa na hati mkato. Kleist alikuwa mwanasiasa wa kuheshimika na aliasisi chombo ambacho ndicho kulichokuja kuasisi TANU. Kleist alikuja kuwa mfanyabiashara na akatajirika. Halikadhalika historia ya mwanae Abdulwahid ilikuwa ya kupendeza iliyojaa matokeo mengi yaliyoendana na historia ya Afrika baada ya Vita Kuu ya Pili. Akiwa katika kikosi cha askari wa miguu huko Burma historia ilionyesha kuwa Abdulwahid alionyesha fikra za kutaka kuwaunganisha Watanganyika chini ya TANU. Fikra hii aliitoa siku ya mkesha wa Krismas mwaka 1945 akiwa Kalieni Camp India pamoja na askari wenzake wakingojea meli kurudi Tanganyika baada ya kwisha vita.
Aliporudi Tanganyika Abdulwahid aliendeleza harakati akiwa katibu wa Dockworkers Union mwaka 1948 hadi alipochukua uongozi wa TAA mwaka 1950 baada ya kifo cha baba yake mwaka 1949. Nyerere akisoma yale aliyokuwa akiandika Abdulwahid alifahamu kuwa kabla ya yeye kushika nafasi ya urais wa TAA nafasi ile Abdulwahid alimuomba Chifu Kidaha Makwaia aichuke lakini Kidaha hakutaka. Hakika maisha yote ya Abdulwahid yalijaa matokeo na visa vya kutosha kuandika kitabu cha historia. Chifu Kidaha na Nyerere walikuja wakawa mahasimu wakubwa na Chifu Kidaha akahamia Kenya .
Inasemekana Nyerere alipokuwa akisioma habari hizi za ukoo wa Sykes ndipo alipomjua kwa undani marehemu Abdulwahid na alijihisi kupwaya katika historia ile. Kweli baba yake alikuwa Chifu wa Wazanaki lakini hakuwa na historia yoyote ambayo angewezanae kuieleza mbele ya watu na watu wakamsikiliza. Hakuna aliyemjua baba yake Nyerere wala hata kama alipata elimu. Abduwahid alikuwa na nyaraka na taarifa za histioria ya wazee wake zilizokwenda nyuma miaka mia moja. Kuanzia Mozambique Kwa Likunyi alipotoka babu yake ambae alikuwa shemeji wa Chifu Mohosh wa Wazulu hadi walipoingia Tanganyika miaka ya mwisho ya 1800 na mchango wao katika kulipigania taifa dhidi ya ukoloni. Historia hii Nyerere aliikataa na kwa hakika ikakatalika hadi leo. Ndiyo maana imefika hadi inakatalika kunasibisha harakati za uhuru na familia ya akina Sykes. Waswahili tuna msemo “Penye ukweli uongo hujitenga.”
Abdulwahid alipotambua kuwa Nyerere hakuwa na nia hasa ya kutafiti na kuandika historia ya kweli ya Tanganyika haraka akajitoa katika kazi ile. Kazi hii alikuwa akiifanyia katika ofisi za TANU ofisi ile ile ambayo aliitumia wakati akiwa rais wa TAA. Inasemekana baada ya hapo Abdulwahid hakukanyaga tena ofisi ya TANU hadi mauti yalipomfika mwaka wa 1968. Lakini kubwa zaidi ni kuwa aliuzuia ulimi wake kusema chochote kuhusu TANU na mchango wake. Hata Lady Judith Listowel [16]aliyeandika “The Making of Tanganyika” alipokuja Tanganyika kufanya utafiti, Abdulwahid hakufungua kifua chake. Hata hivyo Dr Kleruu aliendelea na utafiti na akakamilisha historia ya TANU. Haijulikani mswada wa Klerru uko wapi lakini waliousoma wanasema umefuta mchango mzima wa marehemu Abdulwahid Sykes na mchango mzima wa Waislam katika kuunda TAA na baadae TANU katika kupigania uhuru wa Tanganyika.[17]
Baada ya kupatikana uhuru mwaka 1961 iko siku Mwalimu Nyerere alikwenda ofisi ya TANU. Pale akamkuta Shariff Attas. Mwalimu alimwuliza Shariff Attas wapi wamekutana kwani sura yake inaonyesha kama wanafahamiana. Shariff Attas kwa utulivu akamjibu Nyerere kuwa hawajapata kukutana katika maisha yao. Shariff Attas alikuwa kidogo ameghadhibika akiona kama vile sasa Nyerere kawa rais wa nchi kesha wasahau rafiki zake wa zamani na yeye hakuwa tayari kujipendekeza kwake akamwambia kwa mkato kuwa hawajuani. Lakini kubwa zaidi na la kushangaza ni kuwa Nyerere mwaka 1985 katika hotuba ya kuwaaga wazee wa Dar es Salaam aliokuwanao wakati wa kupigania uhuru alisema kuwa katika vijana waliokuwepo wakati ule alikuwa Dossa Aziz na Abdul Sykes lakini hakumbuki Abdulwahid alikuwa na cheo gani katika TAA.
Inasemekana katika kipindi chake chote alipokuwa madarakani Nyerere hakupata kusikika kuwataja katika hadhira yoyote viongozi wa TAA aliowakuta katika siasa kabla yake. Watu kama Dr. Vedasto Kyaruzi,[18] Dr. Luciano Tsere, Dr. Joseph Mutahangalwa, Dr. Michael Lugazia, Dr. Wilbard Mwanjisi[19] na wengineo. Historia ya harakati za uhuru wa Tanganyika inalazimishwa ianze na Nyerere kiasi kwamba inapotajwa kuwa Nyerere alichukua uongozi wa TAA mwaka 1953 haitajwi kauchukua uongozi huo kwa nani na katika mazingira gani. Inawezekana kweli mtu wa kiwango cha akili ya Mwalimu Nyerere akawa na kumbukumbu fupi kiasi cha kusahau kuwa aligombea nafasi ya urais wa TANU na Abdulwahid Sykes? Siku alipojaribu kumtaja Abdulwahid Sykes ndipo ulimi ukamteleza akasema hakumbuki Abdulwahid Sykes alikuwa na cheo gani katika TAA. Jambo la kusikitisha ni kuwa aliyasema maneno hayo mbele ya wazee wa Dar es Salaam ambao yeye asingewajua sama na Abdulwahid na Dossa. Leo hii si tabu kujua picha aloiacha Mwalimu Nyerere kwa wazee wale. Ilikuwa Nyerere kafika safari yake lakini kasahau kituo alichopandia basi.
Kweli inawezekana vipi Nyerere akawa kasahau uchaguzi ambao ndiyo uliomwingiza yeye katika siasa na uongozi wa Waafrika wa Tanganyika na mwishowe kuupata ubaba wa taifa? Nyerere anaweza kweli kamsahau Shariff Attas dalali wa soko au hata Mzee Abdallah muhudumu wa ofisi ya Abdulwahid lakini vipi Nyerere amsahau rafiki yake Abdulwahid mtu aliempokea Dar es Salaam akaishi nyumbani kwake alipoacha kazi, mtu alieshughulika na safari yake ya kwenda Umoja wa Mataifa kwa niaba ya TANU na mtu aliyemwingiza na kumpa uongozi wa TAA na kumkabidhi majalada na ofisi ya chama achilia mbali ile kumjulisha kwa wanachama na watu mashuhuri wa mjini?
Mwandishi wa makala haya alipoandika kitabu kuhusu maisha ya Abdulwahid Sykes “The Life and Times of Abduwahid Sykes (1924 – 1968) the Untold Story of the Muslim Struggle against British Colonialism in Tanganyika” alimlaumu John Illife ambae aliandika sana kuhusu historia ya Tanganyika kwa kutokuwa makini katika utafiti wake kiasi cha kukosa kuzisoma nyaraka za Sykes na hivyo kuandika historia iliyokuwa na ukweli nusu. John Iliffe alipoandika pitio la kitabu katika Cambridge Journal of African History aliandika kwa hasira na kusema kuwa Abduwahid Sykes hakuasisi TANU. Hata hivyo Jonathan Glassman na James Brenan wanahistoria vijana na mahiri katika historia ya Tanganyika wamesema kuwa si rahisi kwa mtafiti yeyote kupuuza kitabu hicho kwani kimekuja na mengi mapya ambayo hayakuwa yanafahamika kwa wengi.
Kwa kumalizia ningependa kusema kuwa isidhaniwe kuwa kwa kuwapuuza wazalendo wengine na kubadilisha historia ndipo ilipo njia ya kumjenga Nyerere. Kwa kufanya hivyo hawamjengi bali wanambomoa vibaya sana hasa ikiwa sasa Mwalimu Nyerere yuko katika mchakato wa kuwa “mwenye heri” kuelekea kuwa “mtakatifu” kamili. Uongo na udanganyifu si sifa ya utakatifu. Itapendeza ikiwa tutamuenzi Mwalimu kwa yale anayostahili na yapo mengi sana.
21 December 2009
[1] Habari kamili za Abdulwahid Sykes angalia Mohamed Said Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes Historia Iliyofichwa Kuhusu Harakati za Waislam Dhidi ya Ukoloni wa Waingereza,Phoenix Publishers, Nairobi 2002.
[2] Hamza Mwapachu Mdigo kutoka Tanga ndiyo aliyemtambulisha Julius Nyerere kwa Abdulwabid Sykes. Mwapachu allikuwa kati ya waanasiasa wa mwazo wa mrengo wa kushoto na alikuwa na mafungamano na wanaharakati Wazungu katika Labour Party ya Uingereza ambao walikuwa na msimamo mkali dhidi ya ukoloni. Mwapachu alifariki mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 44.
[3] Kuhusu maisha ya Kleist Sykes soma Daisy Sykes Buruku, Kleist Sykes The Townsman katika, Modern Tanzanians, Illife, John (ed), East African Publishing House, Nairobi, 1973.
[4] Denis Phombeah aligombana na Nyerere baada ya uhuru na mwisho akakimbia nchi.
[5] Titi Mohamed alianza kuhutubia mikutano ya TANU katika viwanja vya Mnazi Mmoja kabla hajamjua Julius Nyerere aliingizwa TANU na Schneider Plantan.
[6] Said Chamwenyewe ndiye liyeitafutia TANU wanachama wa mwanzo kutoka Rufiji alikotumwa na Abdulwahid Sykes Julai 1954. Alitoka TANU baada ya kuhitilafiana na Nyerere kuhusu Kura Tatu akamuunga mkono Zuberi Mtemvu katika African National Congress.
[7] Sheikh Suleiman Takadir alifukuzwa TANU kwa kumshutumu Nyerere kuwa uhuru ukipatikana hatawatendea haki Waislam walioupigania uhuru wa Tanganyika. Sheikh Takadir ndiye aliekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU Dar es Salaam.
[8] Iddi Faizi Mafongo na ndugu yake Iddi Tosiri ndiyo waliompeleka Nyerere Bagamoyo Kumtambulisha kwa ndugu yao Sheikh Mohamed Ramia Khalifa wa Tariqa Kadiriyya. Sheikh Ramia na Nyerere wakaja kuwa marafiki wakubwa sana. Iddi Faizi Mafongo ndiye aliyetumwa Tanga na TANU kwenda kuchukua fedha kutoka kwa Mwalimu Kihere kuja kukamilisha nauli ya Nyerere kwa safari ya Umoja wa Mataifa mwaka wa 1955. Special Branch walimkamata njiani Turiani wakamshusha kwenye basi lakini hawakuziona fedha zile na zikafika Dar es Salaam ofisi ya TANU salama.
[9] Mwalimu Stephen Mhando alikataa kufundisha wanafunzi wake kwa mtaaala wa kikoloni na kila alipopata nafasi aliwasomesha wanafunzi wake historia ya kweli ya uzalendo na ushujaa wa Mwafrika. Aligoma kabisa kuwaita Susi na Chuma waliobeba mwili wa David Livingstone kuwa walikuwa watumishi. Yeye aliwaitikadi kuwa walikuwa rafiki wa David Livingstone. Mwalimu Stephen Mhando alikuwa bingwa wa lugha ya Kiingereza na ni mmoja pamoja na Abdwahid Sykes, Hamza Mwapachu, Dr. Vedasto Kyaruzi, Sheikh Hassan bin Amir katika wanakamati wa TAA walioandika Memorundum iliyopelekwa kwa Gavana Edward Twinning mwaka 1949 na hiyo memorandum ikaja kuwa msingi wa hotuba ya Julius Nyerere Umoja wa Mataifa mwaka 1955. Kwa habari zaidi angalia Cranford Pratt, Cranford Pratt, The Critical Phase in Tanzania 1945-1968,Cambridge University Press, London, 1976, uk. 29-31.
[10] Mara ya kwanza kuchapwa historia kinzani na historia rasmi ya uhuru wa Tanganyika ilikuwa mwaka wa 1988. Angalia Mohamed Said, ‘In Praise of Ancestors’ Africa Events,London, March/April 1988, uk. 37-41. Kada wa Chama Cha Mapinduzi akiandika kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma alitoa vitisho kwa mwandishi. Angalia Africa Events, May, 1988, barua ya Dr. K. Mayanja Kiwanuka.
[11] Soma maisha ya Ali Migeyo katika G. Mutahaba, Portrait of a Nationalist: The Life of Ali Migeyo, East African Publishing House, 1969 ndani ya kitabu hicho utapata pia habari za wazalendo wengine kama Sued Kagasheki.
[12] Yusuf Chembera na Salum Mpunga ni waasisi wa TANU Lindi 1956 Mpunga ndiyo aliyomfuata Mwalimu Nyerere Dar es Salaam kuuomba aende Lindi kuhamasisha wananchi kuhusu TANU ni ni wao waliomjulisha Nyerere kwa Sheikh Yusuf Badi.
[13] Hamisi Taratibu na Omar Suleiman ni waasisi wa TANU Dodoma mwaka 1955. Mzee Omar Suleiman amweka kama kumbukumbu kitanda alichukuwa akilalia Mwalimu Nyerere nyumbani kwake wakati wa harakati.
[14] Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 ilitokea sintofahamu baina ya Kasella Bantu na Nyerere na Kasella Bantu akawekwa kizuizini na alipotoka akakimbia nchi kwenda kuishi Ujerumani.
[15] Japhet Kirilo ndiyo alikuwa Mtanganyika wa kwanza kuhutubia Umoja wa Maataifa katika Mgogoro wa Ardhi ya Wameru mwaka 1952. Angalia Kirilo Japhet and Earle Seaton, The Meru Land Case, Nairobi, 1966. Abdulwahid Sykes akiwa katibu wa TAA ndiye aliemsimamia Kirilo kupata hati ya kusafiri kwenda New York baada ya serikali ya kikoloni kumkatalia kumpa pasi. Katika mgogoro huu TAA ilishirikiana kwa karibu sana na Meru Citizen’s Union chama kilichoundwa na watu wa Meru kusukuma mbele madai yao.
[16]Judith Listowel, The Making of Tanganyika, London, 1965.
[17] Kivukoni Ideological College, Historia ya Chama Cha TANU 1954-1977,Dar es Salaam, 1981.
0 comments:
Post a Comment