Home » , » Bibi Titi Mohamed (1926 - 2000) Shujaa wa Uhuru wa Tanganyika

Bibi Titi Mohamed (1926 - 2000) Shujaa wa Uhuru wa Tanganyika

Written By mahamoud on Wednesday, December 25, 2013 | 11:15 PM



Bi. Titi Mohamed (1926-2000)
Utangulizi
Ni vigumu kusema ni lini nimekuja kumfahamu Bi. Titi Mohamed. Nimefumbua macho nikikuwa katika mitaa ya Dar es Salaam ya miaka ya 1950 na 1960 nikimuona na kumfahamu kuwa huyu ndiye Bi. Titi. Mwanamke shupavu na kiongozi wa TANU. Haikunipitikia kwa wakati ule nikiwa bado kijana mdogo wakati mwingine nikimuona katika mikutano ya TANU pale Mnazi Mmoja au Jangwani kuwa ipo siku nitakaa nitafiti historia ya mashujaa wa uhuru wa Tanganyika na Bi. Titi awe mmoja wa mashujaa wangu ambao nilataka sana kuandika maisha yao. Siku moja tu kabla ya kifo cha Bi. Titi nilikuwa nikihojiwa na mwanafunzi wa kike wa Kitaliana kutoka Chuo Kikuu cha Napoli, Italia ambae alikuwa akifanya utafiti kuhusu nafasi ya wanawake katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Binti huyu alikuwa alinihoji kuhusu Bi. Titi na akataka kujua kwa nini hatajiki katika historia ya TANU na kwa nini wanawake wenzake aliokuwa nao katika harakati za kudai uhuru wanaonekana kutopenda kueleza habari za Bi. Titi. Nilimfahamisha binti yule kuwa sisi Watanzania tuna historia rasmi ya uhuru wa Tanzania ambayo tunatakiwa kuienzi. Historia hiyo inaanza na Mwalimu Nyerere na kuishia na Mwalimu Nyerere. Historia hiyo imewatoa wazalendo wengi katika historia pamoja na Bi. Titi. Binti huyo alikuwa na masikitiko kuwa wakati alipofanya mipango ya kutaka kwenda kumuhoji Bi. Titi akamkuta mgonjwa kwa hiyo hakuweza kufanya mahojiano. Nilimfahamisha mtafiti huyu yale niliyokuwa nayajua kuhusu Bi. Titi kisha tukaagana. Siku ya pili nikapata habari kuwa Bi. Titi amefariki.
Kama alivyokuwa akisema mwenyewe marehemu, ‘Yote kuhusu mimi yameshaandikwa nyie waandishi wa leo mtaandika nini ?’ Ni kweli Bi. Titi kaandikwa sana lakini waliomuandika hawakummaliza, kwa kuwa  hawakummaliza ndiyo maana na mimi nimepata nguvu ya kuweza kumuandika lau kama kwa muhtasari. Kwa hakika wengi wa waandishi hao walikuwa wageni ; na wale waandishi wazalendo walipomwandika Bi. Titi walimwandika kwa mtazamo wa agenda zao na vilevile bila kuwa na ujuzi wa historia ya Dar es Salaam katika miaka ya 1950. Wageni walimtazama Bi. Titi kwa jicho la ugeni mimi nataka kumwandika Bi. Titi kama alivyokwenda na historia ya kudai uhuru. Nataka kumueleza Bi. Titi tokea mwanzo alipokuwa na Mwalimu Nyerere. Nyerere akibandua hatua yake unyayo wa Bi. Titi unafuatia. Nataka kumuandika Bi. Titi jinsi alivyopanda kutoka msichana mdogo wa Ki-Dar es Salaam akiwa na miaka 26 hadi kufikia umaarufu mkubwa kabisa. Kisha ghafla nyota yake ikachujuka akaanguka na akaishia kufungwa kifungo cha maisha kwa kosa la uhaini ambalo hadi kufa kwake alikana kuhusika. Nataka kumuandika Bi. Titi jinsi alivyotoka kifungoni akiwa fukara mali yake yote imepotea na jinsi alivyoyakabili maisha ya upweke na kutengwa. Nataka kumuandika Bi. Titi jinsi kwa ufundi mkubwa na subra ya hali ya juu alivyomtegemea Mungu kama nilivyopata kumsikia akisema na Mungu akaitika dua zake na kamrudishia siyo mali zake tu bali hata na hadhi yake. Mtaa aliopewa kwa heshima yake ambao alinyang’anywa ukaja kurudishwa jina lake. Na wale waliomfanyia khiyana ile wakiwa wa hai na hawana uwezo wa kufanya lolote. Vipi Bi. Titi akaja kuuguzwa na kuzikwa na walewale watu waliolitangazia taifa kuwa alikuwa msaliti na ta’azia zao baada ya kifo chake zikajaa maneno ya kumsifu. Ilikuwaje ikawa hivyo?
Nikiwa mtu mzima nilifanyiwa mihadi na Ally Sykes ya kuzungumza na Bi. Titi katika ya miaka ya 1990 nyumbani kwake Upanga. Baada ya kusalimiana na kuniuliza nilikotoka nilimfahamisha wazazi wangu. Nilishangaa kuwa alikuwa anamfahamu baba yangu vizuri sanahata akanieleza wajihi na umbo lake. Nilimfahamisha kuwa nilikuwa nataka kuandika maisha yake. Bi. Titi akanikatalia kwa njia ya kistaarabu kabisa. Kwa hekima kubwa sanaaliweza kunitoa katika mazungumzo ya harakati za siasa za kudai uhuru na akaelekeza fikra zangu katika senema ya watoto Cinderella niliyokuta akitizama pamoja na wajukuu zake. Kwa wale ambao walikuwa karibu na Bi. Titi watakuwa wanajua jinsi alivyokuwa fasaha wa kuzungumza na jinsi alivyokuwa hodari wa kushinikiza hoja zake. Niliishia kunywa soda na kutazama ile senema katika TV kisha tukaagana. Lakini kwangu mimi nilikuwa nimefarajika sana. Miaka michache iliyopita rafiki yangu mmoja alikuwa anamuoa binti ya ndugu yake Bi. Titi na harusi hii ilifanyika nyumbani kwa Bi. Titi Temeke. Hali niliyomkutanayo pale Upanga ilikuwa tofauti sanana nilivyomuona Upanga mara tu alivyotoka kifungoni. Lakini kabla sijaondola Bi. Titi alinifahamisha kuwa hazina yake ya nyaraka za wakati wa kudai uhuru pamoja na picha zake  nyingi za kihistoria zilichukuliwa na askari wapelelezi wakati walipokuja kufanya upekuzi katika nyumba yake kwa ajili ya tuhuma za kupindua serikali zilizokuwa zimemkabili katika miaka ya 1970. Nilisikitishwa na hili kwa kuwa nilijua yeyote atakaekuja kuandika habari za Bi. Titi atakuwa amekosa zana za kumsaidia kumwandika mama huyu kwa usahihi.
Bi. Titi Mohamed alihutubia mkutano wake wa mwanzo katika viwanja hivyo na hii ilikuwa hata kabla hajakutana na Julius Nyerere. Ilikuwaje Bi. Titi akahutubia mkutano wa TANU kabla hata hajakutana na Nyerere au hata kabla Nyerere mwenyewe hajafahamika kwa watu wa Dar es Salaam ?
Bi. Titi Mohamed, Schneider Abdillah Plantan,
John Hatch  na TANU - 1955
Historia ya Bi. Titi inaanza na historia ya mwanzo kabisa ya TANU na historia ya TANU na ya Bi. Titi haijakamilika kama hajatajwa Schneider Abdillah Plantan mtoto wa Affande Plantan. Affande Plantan alikuwa mamluki wa Kizulu aliyekuja na Von Wissman pamoja na askari wengine wa kukodi kutoka kijiji cha Kwa Likunyi - Imhambane, Mozambiquekuja kupigana na Abushiri bin Salim bin Harith aliyekuwa Pangani na Chifu wa Wahehe Mkwawa aliyekuwa na ngome yake Kalenga. Wazalendo hawa waliokuwa wanapinga utawala wa Wajerumani Tanganyika. Halikadhalika historia ya TANU itakuwa haijakamilika kama hujautajwa uwanja wa Mnazi Mmoja mbele ya Chuo cha Watu  Wazima. Hapo ndipo kilipokuwa kilinge cha TANU. Lakini mwaka 1955 wakati TANU inaanza kufanya mikutano yake chuo hicho kilikuwa bado hakijajengwa. Sehemu ile ya mbele ulikuwa ni uwanja tu uliojaa mchanga. Watoto walikuwa wakicheza mpira na kwa wakati fulani ulipata kutumika kama uwanja wa mikutano wakati makuli wa bandari ya Dar es Salaam chini ya chama chao Dockworkers Union walipokuwa wanapambana na dhulma za Waingereza. Uwanja ule ulikuwa ndiyo mahali walipokutana makuli na kufanya mikutano yao ya wazi. Mikutano ya siri ilikuwa katika bonde la Msimbazi shambani kwa Mohamed Abeid. Uwanja wa Mnazi Mmoja ndipo mahali Muislam wa kwanza Mzungu kutembelea Tanganyika katika miaka ya 1940, Dr Shadrack alipofanya mhadhara wake kuwahutubia Waislam wa Dar es Salaam. Mkalimani wake akiwa Mzee Kleist Sykes. Uwanja  huu ndiyo watoto wa Dar es Salaam walipokuwa wakicheza Idi El Fitr baada ya mfungo wa Ramadhani na kusheherejea Idi Kubwa (Idi El Haj). Kwa ujumla mambo mengi ya watu wa Dar es Salaam yalikuwa yakifanyika pale. Haikustaajabisha basi kuwa watu wa Dar es Salaam walifanyia mikutano ya mwanzo ya TANU katika Uwanja wa Mnazi Moja. Ni katika uwanja huu ndipo Bi. Titi alipoanza kuwahamasisha Watanganyika, wake kwa waume wajipinde waung’oe ukoloni katika ardhi ya Tanganyika chini ya TANU. Sasa turudi kwa Schneider Plantan.
Schneider Plantan alikuwa mmoja wa wanachama wa African Association. Kaka yake Mwalimu Thomas Plantan alipata kuwa rais wa TAA. Shneider alikuwa mmoja wa wazee wa TAA ambao walishirikiana na wanasiasa vijana waliochukua uongozi wa TAA mwaka 1950 wakiwa na nia ya kuigeuza TAA kuwa chama cha siasa kamili. Mdogo wake, Ramadhani Mashado Plantan ndiye aliyekuwa akiipa TAA nguvu ya propaganda kupitia gazeti lake Zuhra alilokuwa akilimiliki na kulichapa mwenyewe. Schneider aliwachukulia Waingereza kama adui zake. Katika vita ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) Schneider alipigana dhidi ya Waingereza chini ya uongozi wa Von Lettow Vorbeck, mkuu wa majeshi ya Wajerumani katika Afrika ya Mashariki. Katika vita ile alikuwa na ndugu yake Kleist Sykes. Katika vita ya Dunia ya Pili Shneider alikuwa akipita katika mitaa ya Dar es Salaam akishawishi kusambaza chuki dhidi ya Waingereza waliokuwa ndiyo watawala wa Tanganyika na kuwashawishi wananchi wamuunge mkono Hitler na Mussolini dhidi ya Waingereza. Wakati yeye anafanya haya mdogo wake, Ramadhani Mashado Plantan akawa ameanzisha kijigazeti cha kurasa moja kikiitwa Dunia akawa anafanya propaganda za chinichini dhidi ya Waingereza. Kwa ajili hii Schneider alikamatwa na kuwekwa kizuizini Mwanza.  Mwaka 1950 bila ya hofu Schneider alisimama kidete katika mkutano wa TAA katika Arnautoglo akalazimisha mbele ya ofisa wa Kingereza ufanyike uchaguzi ili uongozi mpya uingie wa vijana wengi wao kutoka Makerere College uingie madarakani kuimarisha harakati dhidi ya Waingereza. Uchaguzi huu ndiyo uliomuingiza madarakani Dr Kyaruzi kama rais na marehemu Abdulwahid Sykes akiwa katibu. Huu ndiyo uongozi uliopanga mbinu za kuunda TANU. TANU ilipokuja asisiwa mwaka wa 1954 Schneider alikuwa mmoja wa wanachama wa mwanzo katika nia yake ile ile ya kupambana na Waingereza. Hii ndiyo historia ya TANU. TANU haikuanza mwaka wa 1954 moto wake ulianza kuwaka kwa chinichini miaka mingi nyuma kabla haujajitokeza. Mwanafunzi wa historia ya Tanganyikia ni lazima azame katika utafiti wa watu walioishi kipindi kile ndipo atakapopata ukweli wa mambo. Si kweli kama wanavyodai wana-historia wa sasa ati TAA kilikuwa chama cha starehe.
Viongozi wapya wa TAA walikuwa na uhusiano na Labour Party ya Uingereza. Ndani ya chama hiki kulikuwa na wanasiasa waliojiita Fabian Society. Hawa walikuwa na mrengo wa kushoto na licha ya kuelewana vyema na viongozi wa TAA halikadhalika waliunga mkono juhudi za taa za kutaka kujikomboa na ukoloni. Mmoja wa viongozi hawa John Hatch alikuja kutembelea Tanganyika kama mgeni wa TANU mara Juni 1955. TANU ilifanya mkutano mkubwa sana Mnazi Mmoja na Hatch akawahutubia wananchi. Inakisiwa takriban wanachama wa TANU na mashabiki wake jumla yao kiasi watu elfu ishirini walijitokeza kwenye mkutano huo. Ali Mwinyi Tambwe alikuwa mkalimani wa Hatch. Denis Phombeah pamoja na katibu mkuu wa TANU, Oscar Kambona vilevile walihutubia halaiki ile. Hatch akiwa anaunga mkono ukombozi wa watu weusi aligundua kuwa TANU haikuwa na tawi la akina mama. Katika dhifa ya chai iliyoandaliwa na TANU kwa heshima yake, Hatch alilieleza tatizo hili kwa Schneider Plantan na John Rupia. Hatch alimwambia Schneider kwamba ili kuwa na chama chenye nguvu TANU isiwaache akina mama nyuma. Hatch alimwambia Schneider kwamba huko Uingereza Labour Party kilikuwa kimejikita kwa wanawake kama moja ya nguzo yake kuu.
Schneider alimwendea Bibi Tatu binti Mzee akamwomba kuanzisha tawi la akina mama kwa ajili ya TANU. Bibi Tatu binti Mzee alimpendekeza Bibi Titi Mohamed ndiye afanye kazi hiyo kwa sababu ya tabia yake ya ucheshi na kupenda kuchanganyika na watu na ukweli kwamba toka hapo alikuwa mwanachama wa ‘Bomba Kusema.’ Akina mama hawa ndiyo chanzo cha Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT uliokuja kuundwa mwaka 1962 na Bibi Titi Mohamed alichaguliwa mwenyekiti wake wa kwanza). Fikra ya watu wengi ni kuwa Bibi Titi aliingizwa TANU na Nyerere. Ukweli ni kuwa Schneider Plantan ndiye aliyemtia Bibi Titi katika siasa na Bibi Titi alihutubia mikutano miwili baada ya ule wa Hatch mnamo Juni, 1955 kabla hajakutana na Nyerere. Bibi Titi alijiunga na TANU pamoja na mumewe Bwana Boi Selemani na wote waliingizwa TANU na Schneider Plantan. Boi Seleman ni mwenye kadi ya TANU namba 15 wakati ambapo Bibi Titi, kama ilivyokwishaelezwa kadi yake ni namba 16.
Vikundi vya taarab mjini Dar es Salaam na nyimbo zao, vyama vya wanawake wa mjini kama Saniyyat Hubbi, Goodluck, Coronation,‘Bomba Kusema’ na vikundi vya lelemama ambavyo vilikuwa na udugu na vikundi vya taarab kama Al-Watan au Egyptian,vilitoa mchango mkubwa sana katika kuwaamsha watu kuiunga mkono TANU. Waliounganisha na kuviongoza vyama hivi vya wanawake na harakati za kudai uhuru walikuwa Bibi Titi Mohamed na Bibi mmoja wa Kimanyema, Hawa binti Maftah. Bibi Hawa binti Maftah, kama kiongozi wa lelemama, alijulikana kwa jina la ‘Queen’. Hakuna hata mtu mmoja Tanganyika nzima, mbali na Nyerere mwenyewe, aliyeweza kuifanya TANU kuwa maarufu kama Bibi Titi Mohamed. Bibi Hawa Maftah ndiye aliyeiingiza kwa mara ya kwanza nyimbo za lelemama ziimbwe katika mikutano ya TANU kama mbinu ya kuhamasisha wananchi kukipenda chama. Vyama vya wanawake Nujum ul Azhar, Waridatil Hubb na Egyptian Club vilivyokuwapo mjini Tabora chini ya wanawake kama Nyange binti Chande na Dharura binti Abdulrahman. Vyama hivi vya akina mama vilisaidia sana kuipa TANU nguvu katika Jimbo la Magharibi. Muziki na ujumbe katika nyimbo zilizotungwa maalum kuinua mioyo ya wanachama wa TANU vilikuwa na athari kubwa, hususani katika wakati ule ambapo serikali ya kikoloni ilimpiga marufuku Nyerere kufanya mikutano ya hadhara. Ili kuepuka kadhia hiyo TANU ilikuwa ikiandaa taarab na Nyere alikuwa akikaribishwa kama mgeni wa heshima. Nyerere alikuwa akisimama kufungua hafla na katika kufanya hivyo alisema maneno machache. Kwa namna hii ule moto wa kudai uhuru ulibaki ukiwaka. Kwa njia hii Nyerere aliweza kuwasiliana na wananchi. Halikadhalika kupitia taarab TANU ilikusanya fedha kwa ajili ya harakati. Kulikuwa na wimbo mmoja wa lelemama ambao uligeuzwa kuwa kama ndiyo mwimbo wa Nyerere, mwimbo huu  na ulikuwa akiimbiwa yeye tu. Mwimbo huo ulikuja kuwa maarufu sana kiasi kwamba ulipoimbwa katika mikutano ya TANU watu wote waliimba kwa pamoja. Mashairi yake yalikuwa kama hivi: ‘Muheshimiwa nakupenda sana, wallahi sina mwinginewe Insha Allah Mungu yupo, Tanganyika tutajitawala’.
Kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja mbele ya Princess Hotel. Kwenye jukwaa lililojengwa kwa miti walikuwa wakikaa wale viongozi wa mstari wa mbele ndani ya TANU - Nyerere rais wa TANU, Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU, Bibi Titi Mohamed, John Rupia na Clement Mtamila. Sahani ya santuri ilikuwa ikipigwa katika gramafoni kupitia kipaaza sauti. Mwimbo uliokuwa ukipigwa ulikuwa wa Frank Humplink. Frank alikuwa kijana wa Kichagga kutoka Moshi. [1] Baba yake alikuwa Mzungu. Hamplink alikuwa mwimbaji na mpiga gitaa maarufu sana wakati ule akipiga muziki wake na dada zake wawili Maria na Regina Humplink. Katika nyimbo zake nyingi Frank alikuwa akiimba pamoja na dada zake. Mwimbo uliopendwa sana na TANU na ndiyo uliokuwa ukipigwa katika kila mikutano yake yote na uliosisimua wananchi ulikuwa na mashairi yafuatayo, ‘Uganda nayo iende, Tanganyika ikichangamka, Kenya na Nyasa zitaumana’. Mwimbo huu ulikuwa na ujumbe wa kisiasa kwa Waafrika wa Tanganyika. Ujumbe katika wimbo huo ulikuwa kuwa, Tanganyika itakapoamka, kutakuwa vilevile na mapambano nchini Uganda, Kenya na Nyasaland. Mwimbo huu ulikuwa ukivuma toka kwenye vipaza sauti mfululizo kabla ya mkutano huku watu wakikusanyika viwanjani. Haikupita muda mrefu serikali ya kikoloni ilipata maana halisi ya wimbo huo. Mara moja mwimbo huo ukapigwa marufuku na serikali.[2] Serikali ya kikoloni iliamuru kwamba mashairi ya wimbo huo yanachochea watu kuasi. Lakini kabla ya mwimbo huo kupigwa marufuku ulipendwa sana na ukwa ukiombwa na wasikilizaji na kupigwa katika kituo cha radio ‘Sauti ya Dar es Salaam’. Kituo hicho cha radio kikaacha kupiga nyimbo hiyo.  Huenda huu ulikuwa wimbo wa kwanza kupigwa marufuku katika historia ya utangazaji Tanganyika. Kwa muda mrefu sana mwimbo huu ulikuwa kama nyimbo rasmi ya TANU. Inaelekea uzalendo na shauku ya uhuru ndiyo vitu vilivyomtia hamasa Humplink hata akatunga na kuimba nyimbo hiyo.
Katika mikutano ya TANU katika zile siku za mwanzo, kabla Nyerere au Bibi Titi kuhutubia umma, Sheikh Suleiman Takadir alikuwa akisimama na kuomba dua. Kwa kawaida alikuwa akisoma ghaibu Surat Fatihah, sura ya kwanza katika Qur’an Tukufu:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu. Kila sifa njema ni milki yake Mwenyezi Mungu, Mola wa Ulimwengu wote. Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu. Mfalme wa siku ya Hukumu. Wewe tu ndiyo tunayekuabudu na wewe tu ndiyo tunakuomba msaada. Tuongoze katika njia iliyonyooka, njia ambayo umewaongoza wale uliowaneemesha, si ya wale uliowaghadhibikia wala ya wale waliopotea.
Hii ni dua ambayo kwa kawaida husomwa na Waislam kabla ya kuanza jambo lolote la kheri. Wakati Sheikh Takadir akisoma dua hii watu walikuwa wima mikono yao juu wakimshukuru Allah. Baada ya hapo Nyerere au Bibi Titi, kutegemea na ujumbe maalum uliotaka kutolewa katika siku hiyo, alikuwa akisimama na kuhutubia.
Bibi Titi alikuwa akijulikana kwa maneno yake makali wakati Nyerere alikuwa bingwa wa fikra tulivu na utoaji wa ujumbe mzito. Sheikh Suleiman Takadir mwenyewe, vilevile alikuwa msemaji mzuri sana. Ilikuwa kwa sababu hii na umri wake mkubwa ndiyo alipewa heshima na wazee wa mji ya kuzungumza kwanza kabla ya yoyote hajasema na kuomba dua, kisha kumtambulisha Nyerere kwa wananchi. Katika siku hizo Nyerere alizoea kuvaa kaptura na soksi ndefu, mavazi yaliyopendwa na walimu wa shule na hasa kivazi kilichopendwa na wale waliojiona wameelimika, hususan watu wenye asili ya bara. Nyerere amenukuliwa akisema kuwa ilikuwa Dossa Aziz ndiye aliyemtahadharisha kuwa maadam sasa anachanganyika na wazee haitakuwa vyema kwake kuonekana amevaa kaptura.
Hotuba hii aliyotoa Nyerere siku ile pale Mnazi Mmoja ambapo aliwaeleza watu  kuhusu safari yake kwenda Umoja wa Mataifa ilikuwa ndiyo mwanzo hasa wa historia mpya ya Tanganyika. Kabla ya hapo Waafrika wa Tanganyika hawakupata kuonyesha shauku na matumaini katika mustakbali wao. Katika viwanja vya Mnazi Mmoja Nyerere aliwaeleza halaiki ya watu wenye furaha na waliokuwa wakimsikiliza kwa makini kuwa miongoni mwa mataifa kumi na mbili yanayounda Baraza la Udhamini saba kati yao yalitoa idhini kuwa muda wa utawala wa ndani wa Tanganyika utakapowadia, Waafrika lazima wapewe nchi yao. Katika hotuba yake Nyerere alitilia mkazo sera ya TANU kuhusu mahusiano mema baina ya Waafrika na watu wa mataifa mengine na aliwaonya wanachama wa TANU ambao walikuwa wameanza kuwabagua watu wa rangi tofauti kuwaambia kuwa hivyo haikuwa sawa. Alisisitiza juu ya umoja miongoni mwa wananachi na hatimaye aliwadhihaki wasikilizaji kwa kuwauliza ikiwa wangesubiri kwa miaka ishirini na tano kuwa huru. Halaiki hiyo ya watu kwa pamoja ilipiga kelele, ‘hapana’. Wananachi kwa pamoja walijibu kwa sauti kubwa wakisema walitaka uhuru kesho au kesho kutwa.[3]
Nyerere ambaye alikuwa akiogopa kuchukua uongozi wa TANU tangu 1953 alikuwa amefarajika sana na mshikamano huu ulioonyeshwa na wananchi. Sasa ilikuwa dhahiri kwake kwamba rafiki yake Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na uongozi mzima wa TANU pamoja na lile Baraza la Wazee lilikuwa limemsafishia njia kuongoza harakati kwa niaba yao. Lakini Padri Walsh na Wamishionari katika shule ya Mtakatifu Francis, Pugu, walitazama harakati hizi kwa mtazamo mwingine kabisa. Wamishionari hawakuweza tena kumvumilia Nyerere kuwa mmoja wa walimu katika shule yao. Hatima ile ile iliyowasibu wazalendo wengine kabla yake sasa ilimkabili Nyerere. Aliambiwa ama abakie mtumishi mtiifu wa kanisa au ajiuzulu; Kanisa halikuweza kukaa kimya na kumuangalia Nyerere akiwatumikia mabwana wawili.
Nyerere alilipeleka tatizo hili kwa Clement Mtamila, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya TANU. Mtamila aliitisha mkutano wa kamati kuu nyumbani kwake mtaa wa Kipata na TANU ilijadili tatizo hilo. Miongoni mwa wajumbe wa kamati ile mbali na Rupia na Kambona walikuwa Bibi Titi Mohamed na Bibi Tatu bint Mzee.[4] Kamati Kuu ya TANU ilimshauri Nyerere ajiuzulu. Tafarani hii ilitokea wiki chache tu baada ya kurudi kutoka Umoja wa Mataifa katika wiki za mwisho za mwezi Machi. Tarehe 23 Machi, 1955 Nyerere alijiuzulu ualimu. Ilikuwa adhuhuri Nyerere alipokuja Dar es Salaam kutoka Pugu, akiwa si mwalimu wa shule tena. Inasemekana aliposhuka tu kwenye basi alikwenda moja kwa moja ofisini kwa Abdulwahid katika soko la Kariakoo kumpasha habari rafiki yake. Nyerere alikaa na Abdulwahid katika nyumba yake namba 78 Mtaa wa Stanley. Baadaye kidogo Nyerere alirudi kijijini kwake huko Musoma. John Hatch alipokuja Dar es Salaam kwa waliko wa TANU Nyerere alikuwa kwao kijijini. Tutaona hapo baadae kidogo jinsi mgeni huyu Mwingereza alivyomgutusha Schneider Abdillah Plantan kuhusu TANU kuwashirikisha wanawake katika harakati za kudai uhuru.
Wanawake na Vyama Vya Lelemama Katika Harakati za Kudai Uhuru
Mwaka 1955 Bibi Titi Mohamed na Julius Nyerere waliitika mwaliko na kuja Tabora. Mkutano ulifanyika katika ile kilabu ya kandanda. Waliohudhuria mkutano ule walikuwa Germano Pacha, Juma Mrisho, Shaaban Mohamed Silabu, Bilali Rehani Waikela, Mohamed Mataka wakati ule akiwa muadhin wa Masjid Nur - msikiti wa Wamanyema pale Tabora, Hassan Mohamed Ikunji, Ramadhani Mussa Wajaku, Swedi Mambosasa, Said Ali Kiruwi na Hamis Khalfan. Uongozi wa kilabu ulimwambia Nyerere na Bibi Titi  kuwa kilabu hiyo ya kandanda ilikuwa ikitaka udugu na TANU ili ifanye kampeni ya kuipatia TANU wanachama wengi. Uongozi huo wa TANU kutoka makao makuu Dar es Salaam uliambiwa kuwa maadam kilabu hiyo ilikuwa ikipendwa na kuungwa mkono na watu wa Tabora na ilikuwa maarufu sana, sifa hizo zingeweza kutumiwa kwa manufaa ya TANU. Vilevile Nyerere alifahamishwa kuwa  kilabu hiyo ingependa kuvijumuisha vyama vitatu vya lelemama na vikundi vya taarabu, Nujum ul Azhar, Waridatil Hubb na Egyptian Club. Nyerere na Titi waliyakubali mapendekezo haya na usiku ule akifuatana na uongozi wa kilabu Nyerere alizungumza na kikundi cha watu waliyokusanyika nje ya nyumba ya kilabu juu ya hali ya Tanganyika katika siku zijazo. Nyerere alikuwa amerudi Tabora ambapo alianza siasa kiasi cha miaka minane nyuma. Jambo muhimu katika kipindi hiki pale Tabora ni kuwa wasomi wa Makerere waliokuwa St. Mary’s School hawakuwapo katika harakati hizi na katika mikakati iliyokuwa ikipangwa. Bibi mmoja wa Kiganda, Nyange bint Chande, mwanachama wa moja ya vikundi vya lelemama mjini Tabora alijitolea nyumba yake kama ofisi ya kwanza ya TANU katika Jimbo la Magharibi. Uchaguzi ulifanyika na Shaabani Marijani alichaguliwa Mwenyekiti wa Wilaya na Idd Said Ludete Katibu wa TANU. Bilali Waikela akawa mjumbe wa kamati. Kadi za kwanza za uanachama wa TANU ziliuzwa ndani ya soko la Tabora  na Amani Idd na Pacha, Katibu wa Jimbo wa TANU. Pacha alikuwa na lingo la kuni pale sokoni kama biashara yake. Baadae Amani Idd alisaidiwa kazi hiyo ya kuuza kadi za TANU na Dharura bint Abdulrahman. Baada ya kufungua tawi la TANU mjini Tanga, uongozi wa chama ulimwalika Julius Nyerere, Bibi Titi Mohamed, John Rupia na Mbutta Milando kufanya ziara Tanga. Nyerere alifikia nyumbani kwa Hamisi Heri. Ujumbe huu kutoka makao makuu ya TANU ulipata makaribisho makubwa yaliyoandaliwa na vyama vya lelemama ambavyo kwa kawaida vilikuwa vingi sana katika pwani ya Afrika ya Mashariki kutoka Mombasa nchini Kenya hadi Mikindani, Tanganyika. Kiongozi wa akina mama hawa mjini Tanga aliyesaidia kuieneza TANU alikuwa Bibi Mwanamwema bint Sultan, ndugu wa mbali wa mwenyekiti wa TANU Tanga, Hamisi Heri. Siku iliyofuata mabingwa wa hotuba wa TANU, Julius Nyerere na Bibi Titi Mohamed walihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Tangamano. Hii ilikuwa hatua kubwa sana kwa TANU, na kwa harakati dhidi ya ukoloni pale Tanga.  Ilikuwa muda mrefu umepita tangu zile siku za zile siasa za wasomi katika Discussion Group, kikundi cha majadiliano; na ile mizozo baina yao na ule uongozi Waarabu katika TAA. Baada ya hapo, Mwalimu Kihere alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TANU Tanga badala ya Hamisi Heri na Amos Kissenge alichaguliwa katibu. Abdallah Rashid Sembe mmoja wa wanachama waasisi wa mwanzo kabisa wa TANU alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU akiwakilisha Jimbo la Tanga.
TANU katika Mombasa, Kenya, 1957
Mambo yalikuwa yanageuka dhidi ya Waingereza katika makoloni yake yote Afrika ya Mashariki. Wazalendo walikuwa wakifanya harakati zao na kuvuka mpaka mmoja wa nchi hadi mwingine bila matatizo. Ule wakati wa wao kusafiri kwa kificho na kufanya mikutano yao nyakati za usiku mafichoni ulikuwa umepita. TANU ilikuwa na nguvu ya sasa kuangali nje ya mipaka yake. Katika pwani ya Kenya katika mji wa Mombasa, kijana mmoja kutoka Moshi, Ismail Bayumi, aliyeajiriwa na Mombasa Municipal Council akivutika na mwenendo wa matukio ya kisiasa kama yalivyokuwa yakitokea katika Afrika Mashariki, aliwashawishi Watanganyika waliokuwa wakiishi na kufanya kazi Mombasa kuunda kile kilichokuja kujulikana kama Mombasa TANU Club. Sheria ya Kenya haikuwaruhusu Watanganyika kuunda chama cha siasa katika ardhi ya Kenya, kwa hiyo TANU Club ilisajiliwa kama chama cha starehe na ilikuwa na ofisi zake katika Barabara ya Lohana. Ismail Bayumi alichaguliwa rais wake wa kwanza. Lakini kwa hakika TANU Club ilifanya kazi kama chama cha siasa kwa niaba ya TANU, KANU na KADU kwa kiwango fulani.  Wakati huo Jomo Kenyatta alikuwa Manyani akitumikia kifungo cha miaka saba gerezani kwa kuhusika na harakati za Mau Mau.
Tom Mboya aliitumia TANU Club kuifanyia kampeni KANU na kupigania kufunguliwa kwa Kenyatta kutoka gerezani. Kote nchini Kenya KANU ilikuwa ikiibuka kama chama cha wananchi wote. Wakati sera za KANU zilikuwa zile za mwelekeo wa kuwaunganisha wananchi wote dhidi ya ukoloni, KADU chini ya Ronald Ngala, kwa upande mwingine, ilikuwa na labda isemwe, ufahamu mfinyu, KADU ikifungamanisha sera zake na siasa za ukabila na utawala wa majimbo. Kwa hiyo KADU ilikuwa ikikusanya nguvu za upinzani wa makabila madogo dhidi ya KANU. KANU chini ya Kenyatta, Jaramogi Oginga Odinga na Tom Mboya, ilichukuliwa kuwa ni chama cha makabila mawili makubwa nchini Kenya, yaani Wakikuyu na Wajaluo ambayo yakiachiwa kutawala yatameza makabila madogo. Nchini Tanganyika ambako ushindani wa kikabila katika siasa haukuwepo, TANU Club ilijikuta kiitikadi inapenda kuwa karibu zaidi na KANU kuliko KADU.
TANU Club ilikuwa ikiandaa dansi katika Ukumbi wa Tononoka na dansi hizi zilikuja kupendwa sana na wanasiasa wa Kenya. Ilikuwa chini ya pazia la sherehe hizi katika Ukumbi wa Tononoka ndiyo wanasiasa wa Kenya na wale wa TANU Club walipata nafasi kupashana habari namna TANU ilivyokuwa ikiendelea nchini Tanganyika na nini TANU ingeweza kufanya huko Tanganyika ili kusaidia harakati za kudai uhuru nchini Kenya. Baada ya TANU Club kufanikiwa sana huko pwani uongozi wake uliamua kufungua tawi la TANU Club mjini Nairobi katika sehemu ya Pumwani. Tom Mboya na Ronald Ngala walikuwa mstari wa mbele katika sherehe zote za TANU Club, wakishiriki katika shuguli zake Mombasa na Nairobi.
Msukumo mkubwa wakati ule nchini Kenya ilikuwa kufanya kampeni ya nchi nzima kuwashinikiza Waingereza wamwachie huru Kenyatta aliyekuwa akichukuliwa na wananchi wote kama kiongozi na nguvu ya umoja wa Waafrika wa Kenya. Katika wimbi hili la kutaka Kenyatta afunguliwe kutoka gerazani, Tom Mboya alimdokeza Ismail Bayumi kuwa TANU ingeweza kusaidia katika kampeni hii ya kuwashinikiza Waingereza kumtoa Kenyatta kifungoni. Ismail alifikisha wazo hili makao makuu ya TANU mjini Dar es Salaamkwa kupitia mtu maalum aliyekuwa akiwasiliana na Tom Mboya na Nyerere kwa siri. TANU ilimtuma Bibi Titi Mohamed kwenda Kenya kuzitia shime harakati za kufunguliwa Kenyatta. Wazalendo nchini Kenyawalikuwa wameshindwa kabisa kuwaingiza wanawake ndani ya KANU hivyo kuzinyima harakati za uhuru nguvu kubwa sanana ya kutegemewa ya akinamama. [5] Huko Mombasa TANU Club ilifikiria kuwa kumleta Bibi Titi kuja Kenya kuifanyia kampeni KANU ilikuwa ni kitu kipya cha kuwahamasisha wanawake ndani ya KANU na kwa hiyo kuongeza nguvu mpya na kutia ari ya utaifa katika Kenya.
Bibi Titi alikuja Mombasa na kufanya mkutano Ukumbi wa Tononoka. Kwa kawaida kwa madhumuni ya kupata kibali mikutano hii ilikuwa inahesabiwa kama ni mikusanyiko ya kufanya sherehe siyo mikutano ya siasa na ilikuwa ikifanyika ndani. Lakini mkutano huu ulikuwa na umuhimu wake kwa sababu ya kuwako Bibi Titi Mohamed mjini Mombasa. Wengi walikuwa wamemsikia Bibi Titi lakini hawakuwa wamepata  kumuona. Watu walijaa ndani ya ule ukumbi hadi nje kuzunguka viwanja vya Ukumbi wa Tononoka. Kwa kweli kwa hali yoyote mkutano ule usingeweza kuitwa kuwa ni mkutano wa wanachama wa TANU Club mjini Mombasa, au hata mkutano wa TANU Club Kenyanzima, kwa sababu wanachama wa KANU waliwazidi wanachama wa TANU Club kutoka Tanganyika.
Kenyailikuwa bado haijaweza kumtoa hata mwanamke mmoja wa kiwango cha Bibi Titi. Kwa wakati ule kumwona mwanamke wa Kiislamu amesimama bila baibui akihutubia halaiki ya wanaume ilikuwa ni jambo la kushangaza sehemu za pwani, ambako wanawake walitembea huku wamejifunika mabaibui na hawakutakiwa hata kufanya kazi maofisini. Bibi Titi alifanya mikutano kule Mombasana Nairobiakiwasisitizia watu wasikate tamaa wasimame pamoja hadi Kenyatta amefunguliwa kutoka gerezani. Habari za mikutano hii iliandikwa kwa mapana na marefu na magazeti ya Mombasa Times na Taifa Leo.
Miongoni mwa Wakenya kule pwani waliyofanya kazi karibu sana na TANU Club walikuwa Msanifu Kombo na Abdallah Ndovu Mwidau. Kombo na Mwidau kwa sababu ya mchango wao kwa KANU kupitia chama chenyewe na kupitia TANU Club wakaja kuwa na ushawishi mkubwa kwa Rais Kenyatta. Wazalendo hawa wawili baada ya uhuru wa Kenyawakawa watu wenye sauti kubwa kule pwani. Hakuna mtu kutoka pwani alikuwa anaweza kuteuliwa na kushika nafasi yoyote muhimu na Kenyatta bila Abdallah Mwidau na Msanifu Kombo kumuunga mkono. Mara tu baada ya kufunguliwa kutoka gerezani, Kenyatta alikwenda Mombasakutoa shukrani zake kwa Msanifu Kombo, Abdallah Mwidau na TANU Club kwa msaada wao kwa KANU na kwa kufanya kampeni ya kufunguliwa kwake. Mkutano ulitayarishwa kule Tononoka na Kenyatta alikuja kutoa hotuba ya shukrani na kukutana na wanachama wa TANU Club.
Ujumbe wa Nyerere mwenyewe kutoka makao makuu ulikuwa na watu wengi ambao wasingeweza hata kidogo kusimama kamawagombea katika uchaguzi chini ya masharti yale. Makao makuu ya TANU yalikuwa yanawakilishwa kwenye mkutano mkuu na Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa Aziz, Julius Mwasanyangi, Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee Salum, Idd Faiz Mafongo, Idd Tosiri, Haidari Mwinyimvua na Rajabu Diwani. Hii ilikuwa na maana uongozi wa Waislam kule Dar es Salaam, Tanga, Tabora, Dodoma na mahala pengine nchini Tanganyikausingeweza kusimama kama wagombea uchaguzi ili wachaguliwe kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria wala wasingeweza kuwapigia kura wagombea wanaowataka. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo la wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi. Serikali ya kikoloni, ikishirikiana na wamishionari, walikuwa wamewanyima Waislam elimu, sharti lile lile ambalo sasa linawekwa kuwazuia Waislam kushiriki katika siasa. Mkutano wa Tabora ulikuwa uamue ikiwa TANU itashiriki katika uchaguzi na kushindana na UTP au ingesusia uchaguzi huo na hivyo kumpa mshindani wake mkubwa na hasimu wake ushindi wa bure.
Hakuna kumbukumbu zozote zinazoeleza mawazo ya Nyerere katika suala la kura tatu wala hakuna nyaraka inayoweza kueleza kuwa alipata hata kuzungumza suala hili kwa faragha pale makao makuu na viongozi wenzake kama Sheikh Suleiman Takadir, Zuberi Mtemvu, Rajab Diwani, Idd Faiz, Haidar Mwinyimvua, Dossa Aziz au Bibi Titi Mohamed. Kwa ajili hii ni vigumu kuweza kujua ni kwa kiasi gani Nyerere alikuwa amejizatiti katika msimamo wa TANU kuingia katika kura tatu chini ya masharti yale. Lakini ikiwa utafanya tathmini kutokana na hali ya hewa ya siasa kama ilivyokuwa katika miezi ya mwisho ya mwaka 1958, si vigumu kuona kwa nini Nyerere ilibidi afiche msimamo wake katika suala la kura tatu kama TANU lilivyotwishwa na serikali. Nyerere alikuwa anafahamu hatari iliyokuwa ikinyemelea TANU kutokana na kura tatu. Alijua wazi ili kukinusuru chama na mgawanyiko kulikuwa na haja kubwa ya yeye kufanya uamuzi haraka na kwa makini kabla ya kuenda kwenye mkutano Tabora.
Siku kadhaa kabla ya kusafiri kwenda Tabora kwenye ule mkutano mkuu wa mwaka wa TANU, Nyerere na Amos Kissenge, Kaimu Katibu Mwenezi wa TANU, walisafiri kwenda Tanga kushauriana na uongozi wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU Tanga kuhusu matatizo yaliyoletwa na uchaguzi wa kura tatu. Mkutano huu baina ya Nyerere, Kissenge na ule uongozi wa Tanga ulikuwa wa siri sana. Tanga iliwakilishwa na Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Abdallah Rashid Sembe, Ng’anzi Mohamed, Mustafa Shauri na Abdallah Makatta. Nyerere alizungumza waziwazi na kwa ithibati ya moyo wake. Nyerere alikiambia kikao kile kuwa amekuja Tanga kuomba wamuunge mkono kwa sababu ilikuwa ni matakwa yake TANU lazima ishiriki katika ule uchaguzi wa kura tatu uliokuwa unakaribia hata masharti yakiwaje. Nyerere aliuambia uongozi wa Tanga uliokuwa ukimsikiliza kwa makini kuwa alikuwa amekuja kwao kwa sababu watu wa Tanga wanajulikana kwa ufasaha wa lugha na kwa uwezo wao wa kuzungumza vizuri. Nyerere alisema angehitaji hiki kipaji adimu cha watu wa Tanga kuunga mkono msimamo wake huko Tabora. Nyerere alitoa hoja kwamba TANU lazima iingie katika uchaguzi kwa sababu kuususia ni sawasawa na kukipa chama hasimu, UTP ushindi bila jasho kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. TANU ingedhoofika na hivyo ingekosa sauti katika maamuzi yatakayotolewa na serikali katika  siku zijazo.
Kufichuka kwa msimamo wa Nyerere wa kutaka TANU iingie kaatika kura tatu kulishtua uongozi wa Tanga. Majadiliano makali yalifuata uongozi wa Tanga ukionyesha upinzani wao kwa msimamo wa Nyerere. Baada ya majadiliano ya muda mrefu Nyerere alifanikiwa kuwashawishi wote wawili, Hamisi Heri na Mwalimu Kihere ambao ndiyo walikuwa wapinzani wakubwa wa msimamo wa Nyerere na uchaguzi wa kura tatu. Nyerere aliutahadharisha uongozi wa Tanga kuwa agenda ya kura tatu itakapokuja anatabiri kupata upinzani mkali kutoka katika majimbo. Huko Tanga kwenyewe, TANU ilikuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka UTP na serikali. Matawi kadhaa yalikuwa yamepigwa marufuku. [6]  UTP ilikuwa na nguvu Tanga kwa sababu wanachama wake wengi walikuwa wakimiliki mashamba ya mkonge katika jimbo hilo. Kwa ajili hii chama kilikuwa kinaelemewa na mashambulizi kutoka wa wapinzani. Wakati huo Tanga ilikuwa imetoa viongozi wenye uwezo lakini wote walikuwa wamehamishiwa makao makuu mjini Dar es Salaam. Wapangaji mikakati wazuri kama Peter Mhando alikuwa amehamishiwa Dar es Salaam na kutoka hapo alipelekwa Tabora ambako si muda mrefu akafa. Elias Kissenge vilevile alihamishiwa makao makuu kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa TANU baada ya Oscar Kambona aliyekuwa ameshika nafasi hiyo kwenda Uingereza kwa ajili ya masomo. Uongozi wa TANU Tanga hata baada ya kujadili mbinu waliyopanga na huku Nyerere akielekeza mikakati ambayo Mwalimu Kihere na Abdallah Rashid Sembe wataitekeleza Tabora, bado uongozi ule ulikuwa na wasiwasi wa mafanikio ya mpango huo. Kwa ajili ya wasiwasi huu, viongozi wa TANU wa Tanga walimuomba Nyerere wawe pamoja ili ifanywe tawaswilwaombe msaada wa Allah awape ushindi dhidi yaa vitimbi vya Waingereza. 
Maili tatu kutoka Tanga kipo kijiji cha Mnyanjani ambako kulikuwako na tawi la TANU lililokuwa na nguvu sana likiongozwa na Mmaka Omari kama mwenyekiti na Akida Boramimi bin Dai akiwa katibu. Mmaka alikuwa kijana aliyekuwa akiendesha mgahawa pale kijijini na Akida bin Dai alikuwa mwashi. Akida aliongoza tawi la vijana wa TANU ambalo baadae lilikuja kujulikana kama Tanga Volunteer Corps (TVC). TVC ilikuwa sawasawa na Bantu Group, ambayo wakati huo ilikuwa imekwishaanzishwa huko Dar es Salaam na Tabora. Vikundi hivi mbali na kufanya shughuli za propaganda na kuhamasisha wananchi halikadhalika viliifanyia TANU ujasusi. Nyerere na Kissenge walichukuliwa hadi Mnyanjani na tawaswil ikasomwa. Waliohudhuria kisomo hicho  walikuwa Abdallah Rashid Sembe, Sheikh Dhikr bin Said, Mzee Zonga, Hemed Anzwan, Salehe Kibwana aliyekuwa mshairi maarufu, Akida Boramimi bin Dai na Mmaka Omari. Aliyechaguliwa kusoma Quran Tukufu alikuwa mjomba wa Mwalimu Kihere, Sheikh Ali Kombora.
Mjadala wa Kura Tatu
Wasomi waliokuwa Dodoma, Tabora na Tanga walishindwa kabisa kuunda chama cha siasa. Kazi hii ilitwikwa na kubebwa kwa mafanikio makubwa na Waislam ambao hao waliokuwa na kisomo waliwaona ni wachache wa elimu. Hadi kufikia mwaka wa 1958, TANU ilikuwa na nguvu na ilikuwa ipo takriban kila jimbo nchini Tanganyika na ilikuwa sasa inatarajia kushiriki katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia. Hapakuwa na shaka yoyote kuwa TANU ingesusa kushiriki katika uchaguzi wa kura tatu kwa sababu ya masharti ya kibaguzi yaliyowekwa na serikali ya kikoloni. Waafrika hawakuweza kutimiza masharti yale hasa Waislam ambao ndiyo walikuwa mstari wa mbele katika harakati za kumng’oa Mwingereza kutoka Tanganyika. Hii ilimaanisha kuwa Waislam waliokuwa viongozi katika TANU wasingeweza kusimama wapigiwe kura kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria na halikadhalika halaiki ya Waislam waliokuwa katika harakati za siasa wasingeweza halikadhalika hata kupata ile haki ya kupiga kura.
Uchaguzi wa kura tatu ulikuwa ukizuia uongozi wa kuchaguliwa na watu kuingia kwenye madaraka. Viongozi kama Sheikh Suleiman Takadir, Fundi Mhindi, Omar Suleiman, Hamis Heri waliochaguliwa na watu kidemokrasia kuongoza harakati dhidi ya mfumo dhalimu walikuwa wanapigwa marufuku kushiriki katika mustakabali wa nchi yao kwa matakwa ya wakoloni tu wala si kwa sababu yoyote ile ya msingi. Katika hali kama hii yale yote ambayo Waislam waliojitolea mhanga kwayo, yalionekana kama yamepotea bure. Mara baada ya kurudi kutoka Tanga Nyerere aliondoka kwenda Tabora akiongoza ujumbe mkubwa sana kutoka makao makuu ndani yake wakiwemo: Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa Aziz, Julius Mwasanyangi, Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee Salum, Idd Tosiri, Hadari Mwinyimvua, Rajab Diwani na wengine.
Katika miaka ya 1950 Tabora ulikuwa mji mdogo usiokuwa na uwezo wa kuhimili ugeni kwa ujumbe mkubwa kama ule wa TANU ambao ulitoka majimbo yote ya Tanganyika. Ofisi ya wilaya ya TANU, Tabora, sasa chini ya uwenyekiti wa Mohamed Mangiringiri, fundi cherahani aliyeajiriwa na mfanyabiashara wa Kiasia, G. B. Somji, iliwashirikisha wanachama wote na vyama vilivyokuwa na udugu na TANU kwa kuwaomba wachange kwa ukarimu fedha ili kufanikisha mkutano ule na vilevile wachangie chochote watakachoweza kutoa kwa ajili ya kuwakimu wageni. Wanachama walitoa nyumba zao kwa ajili ya malazi ya wajumbe, wengine walitoa vyakula, mablanketi, shuka, magodoro na samani. Wale matajiri walijitolea fedha taslimu. Usalama wa wajumbe ulikabidhiwa kikundi cha TANU Bantu Group. Ramadhani Abdallah Singo, [7] wakati huo akiwa na umri wa miaka ishirini na nane na aliyekuwa na sifa ya ubabe na Abdallah Saidi Kassongo, akiwa na umri wa miaka ishirini na nne wote wawili wanachama wa Bantu Group walikabidhiwa kazi ya kumlinda rais wa TANU, Nyerere mara tu atakapokanyaga ardhi ya Tabora.
Issa Kibira, mwanachama muasisi wa tawi la African Association mjini Tabora na sasa mwanasiasa mkongwe na mwenye kuheshimiwa alijitolea kumkaribisha Nyerere nyumbani kwake. Makamu wa rais wa TANU John Rupia na Michael Lugazia walilala katika nyumba nyingine ya Kibira. Kijana mmoja kwa jina Jaffari Idd alichaguliwa maalum kumpikia chakula Nyerere. Mwaminifu kama alivyokuwa, Jaffari alilazimika kula yamini - kiapo cha Kiislamu, kuwa hatashawishika kwa namna yoyote ile na katika hali yoyote kumruhusu adui amshawishi kumtilia Nyerere sumu katika chakula. Jaffari alikumbushwa na wale waliomlisha yamini kuwafikiria Waafrika milioni tisa nchini Tanganyika waliokuwa wanamtegemea Nyerere kama mkombozi wao.
Mnamo tarehe 28 Januari, 1958 Nyerere na ujumbe wake kutoka Dar es Salaam waliwasili Tabora kwa gari moshi. D.C. wa  alikuwa ameionya TANU mapema na katika wakati wa kutosha kabisa kuwa TANU isipeleke zaidi ya watu wawili kumpokea Nyerere na ujumbe wake. Kwa hiyo TANU ilipanga kumpokea Nyerere na wajumbe wengine Igalula, stesheni ndogo nje ya Tabora. Kundi kubwa lililokusanyika Igalula lilimpokea Nyerere na  ujumbe wa TANU toka makao makuu kwa vifijo na nderemo. Baada ya hapo kundi lile la wananchi lilimsindikiza Nyerere na ujumbe wake kwa maandamano makubwa hadi kwenye ofisi ya TANU katika mtaa wa Usagara. Mwaka 1955 Nyerere na Bibi Titi walipokaribishwa Tabora na Young New Strong Football Club hapakuwepo na kishindo chochote. Waliojua kuwa Nyerere na Bibi Titi walikuwapo mjini walikuwa wale waliokutananao uso kwa uso. Safari hii kuja kwa Nyerere Tabora kulikuwa ni ushindi kwa TANU na kishindo chake kilisikika katika wilaya zote nane za Jimbo la Magharibi na nje ya mipaka yake. Zaidi ya wajumbe mia moja na hamsini kutoka kila pembe ya Tanganyikawalikutana Parish Hall, ukumbi wa Kanisa Katoliki kujadili uchaguzi wa kura tatu. Tabora iliwakilishwa na Mzee Fundi Mhindi, Mohamed Mangiringiri na Dharura bint Abdulrahman.
Ile agenda ya uchaguzi wa kura tatu ilipoanza kujadiliwa, mkakati wa Tanga ukaanza kutekelezwa. Nyerere aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano aliomba amwachie kiti Mwalimu Kihere ili apate fursa ya kushiriki katika mjadala na kutoa  mchango wake. Mara tu baada ya Mwalimu Kihere kuchukua kiti aliutuliza mkutano na akamchagua Abdallah Rashid Sembe kuwa msemaji wa kwanza kamavile walivyopanga kule Tanga majuma machache yaliyopita. Sembe alihimiza TANU kushiriki katika uchaguzi. Kama vile Nyerere alivyotabiri mapema, zogo kubwa lilizuka. Wajumbe walipiga makelele, wakagonga meza kwa hasira, wengine wakawa wanaburuza meza na viti kwa fujo kudhihirisha hamaki zao. Jumanne Abdallah, aliyekuwa akifahamika kwa umaarufu wa kuwa Kadiani na Bhoke Munanka kutoka Jimbo la Ziwa walisimama na kumlani Sembe wakimwita msaliti. Sembe alishikilia msimamo wake kuwa TANU ni lazima iingie uchaguzi unaokuja ili ishinde uchaguzi na katika ushindi huo iwe na uwezo wa kufutilia mbali mfumo huo wa kuchukiza. Nyerere alisimama na akamuunga mkono Sembe. Nyerere alitoa hoja katika misingi hiyo hiyo kuwa ili TANU iweze kuondoa kura tatu ni lazima kwanza iingie kwenye kura tatu. Wajumbe hawakuafikiana hoja ile. Wote walishikilia msimamo wa TANU kususia uchaguzi. Hamaki za watu zilikuwa wazi ndani ya ukumbi wa mkutano na Mwalimu Kihere aliahirisha kikao hadi siku ya pili ili kuwapa wajumbe muda wa kutuliza hasira.  Wajumbe walipokuwa wanarudi kupumzika majumbani walikofikia, ujumbe wa Tanga, na hasa Sembe aliyejiletea balaa kwa matamshi yake ndani ya mkutano aliamini kuwa ule mkakati waliopanga na Nyerere ulikuwa unawageukia na kuwa msiba mkubwa na wa kutisha kwake yeye mwenyewe binafsi na kwa chama.
 Siku iliyofuata ustadi wa Nyerere katika mjadala uliokuwa maarufu toka alikupokuwa mwanafunzi Makerere College - ulitumika. Nyerere akizungumza kwa vitendawili na methali, aliwauliza wasikilizaji wake, je, ingewezekana kwa mkulima mwenye busara, aliyelima na kupanda shamba lake kwa taabu, angesita kuvuna mazao yake kwa kuhofia kuchafua nguo zake, kwa sababu tu, ili afike shambani kwake itabidi avuke mto wenye matope. Watu wangelimuonaje mkulima kama huyo? Nyerere aliwaeleza wale wajumbe kuwa, TANU iko njia panda, ingekuwa kazi bure kwa wakati huu kwa chama kususia uchaguzi baada ya kufanya kazi yote ile kwa shida kubwa hadi kufika hapo walipofika. Kusuia uchaguzi ingekuwa ni kujiingiza katika mtego. Adui angefurahi kuona imenasa katika mtego, TANU ikisimama pembeni na UTP ikiingia katika uchaguzi na kuchukua viti vyote katika Baraza la Kutunga Sheria. Serikali ya kikoloni ingefurahi sana kuona kitu hiki kinatokea. Hata hivyo agenda ya kura tatu ilibidi ipigiwe kura. Kura ilipopigwa kundi la msimamo mkali waliotaka kuususia uchaguzi walishindwa: kura thelathini na saba zilipigwa kuunga mkono kushiriki uchaguzi wa kura tatu dhidi ya ishirini na tatu zilizotaka ususiaji. [8] Nyerere na Sembe ambaye alihatarisha uhali wa yeye kuwapo  katika TANU katika suala la uchaguzi wa kura tatu walikuwa washindi.
Baada ya kura kutangazwa Nyerere aliwaambia wajumbe wa mkutano kutoka nje ili wapige picha ya pamoja. Wajumbe wachache sana walikubali, wengi wao waliamua kukaa pembeni wasitokee katika picha kwa hofu ya kuandamwa na serikali. Nyerere alitia sahihi Azimio la Tabora ambalo baadae lilikuja kujulikana kama ‘Uamuzi wa Busara’; siku ile Nyerere alipokuwa akiweka sahihi yake watu hawa wafuatao ndiyo walikuwa wamemzunguka: kwa upande wa kulia wa Nyerere alikuwa amesimama makamu wa rais wa TANU, John Rupia; upande wake wa kushoto alikuwepo Amos Kissenge; aliyekuwa kakaa nyuma ya Nyerere amevaa kofia ya mkono, koti na kanzu alikuwa Mzee Jumbe Tambaza, mjumbe wa Baraza la Wazee wa TANU, upande wake wa kuume alikuwa kijana Juma Selemani maarufu kwa jina la lake la utani, ‘Juma Mlevi’, katibu wa TANU Bantu Group. Waliokuwa wamekaa mwisho wa meza wakitazamana alikuwa Bibi Titi Mohamed kwa upande wa kulia  wa Nyerere na Sheikh Suleiman Takadir kwa upande wake wa kushoto.
Mambo yakawa yamevurugika zaidi kwa kuwa rais wa EAMWS, Tewa Said na makamo wake Bibi Titi Mohamed walikuwa katika baraza la mawaziri la Nyerere na wakapoteza nyadhifa zao za ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1965. Kwa ajili hii basi serikali ikawa inaeneza propaganda kuwa kwa kuwa Tewa na Bibi Titi walikuwa katika uongozi wa juu wa EAMWS, walikuwa wanatumia nafasi zao kujijengea himaya mpya kutoka kwa Waislam dhidi ya Nyerere. Viongozi hawa ikawa lazima washughulikiwe na kuangamizwa. Mtu wa kufanya kazi hii hakuwa mwingine ila Adam Nasibu katibu wa EAMWS Bukoba, mwalimu wa shule ya msingi ambae elimu yake wala haikuwa kubwa. Adam Nasibu alikuwa tayari keshafanikiwa kufanya mapinduzi dhidi ya rais wa EAMWS, Tewa Said Tewa. Kutokana na vitendo vyake alikuwa ameidhihirishia serikali kuwa yeye angeweza kuwa mtumishi bora kwa dola kuliko ule uongozi wa EAMWS uliokuwa pale makao makuu Dar es Salaam ambao ulikuwa ukionekana umechoka.
Wakazi wa Dar es Salaam kila mwaka walikuwa wakifanya maulidi katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW). Huu ndiyo toka asili ulikuwa uwanja ambao TANU ilifanya mikutano yake yote wakati wa kupigani uhuru. Mwezi Juni 1968 maulidi mbili katika usiku mmoja zilisomwa kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume (SAW).  Maulidi moja ilisomwa Mnazi Mmoja na nyingine Ilala. Chanzo cha haya yote ni kuwepo kwa kutoelewana kati ya viongozi wa Waislam waliokuwa wanajiona kuwa ni ‘wazalendo’ wafuasi wa TANU na wale na wale viongozi wa EAMWS ambao kambi nyingine ilikuwa ikiwaona kama wapinzani wa TANU. Yale maulidi yaliyosomwa Ilala yalihudhuriwa na viongozi wa EAMWS na yalipata watu wengi na yakafana sana ukilinganisha na yale maulidi ya Mnazi Mmoja, ya wafuasi wa TANU. Uongozi wa TANU ulitishika na hali hii iliyokuwa ikijitokeza kwa maana ilikuwa inaonyesha kuwa chama kilikuwa kinapoteza wafuasi ambao walikuwa  wakijiunga na kambi ya Tewa na Titi iliyokuwa ikisemekana ipo dhidi ya Nyerere. [9]
Pambano kati ya Nyerere, Tewa na Bibi Titi, 1968
Ili tume ya uchunguzi ya Waislam iweze kufanya kazi yake vyema na bila upendeleo, ilikuwa lazima ile tume ya Waislam iiombe serikali izuie propaganda iliyokuwa ikiendeshwa na wale waliokuwa wamejitenga na EAMWS, wakitumia jukwa la radio ya serikali na magazeti ya TANU. Tume ya Waislam ilikutana na Waziri wa Habari na Utangazaji, Hasnu Makame, ofisini kwake tarehe 20 Novemba, 1968, kujadili tatizo lile. [10] Hii haukusaidia kitu. Propaganda dhidi ya uongozi wa EAMWS iliendelea kwa nguvu zote. Mashambulizi kutoka pande tatu yaliyopangwa vyema yalikuwa kazini. Benjamini Mkapa akitumia gazeti la Nationalistataandika habari yoyote ya Adam Nasibu, Martin Kiama akitumia Radio Tanzania atatumia habari ile kama habari muhimu katika radio na habari hiyo itatangazwa kutwa nzima huku ofisi ya rais ikiwa kimya kwa fitna ile. Lile kundi la waliojitenga na umma wa Waislam Adam Nasibu akiwa kama msemaji wao mkuu wakawa wakati mwingine kwa mastaajabu makubwa wakawa wanakiuka hata misingi ya akida ya Tanzania, wakitoa madai ya ubaguzi a rangi, wakikazania lazima EAMWS ivunjwe. Adam Nasibu alinukuliwa na The Nationalist akisema kuwa:
Waislam lazima wafahamishwe kwa nini East African Muslim Welfare Society iwe na katiba ambayo inaendana na mwelekeo wa nchi. Hatujui nafasi ya Aga Khan katika nchi yetu na ndiyo maana tunamkataa. [11]
Lakini cha kushangaza zaidi ilikuwa ule ukimya wa serikali kuhusu matakwa ya kundi la Adam Nasibu lililokuwa likidai kuwa Waislam wachanganye dini na siasa katika suala hili, wakati ilikuwa ikijulikana wazi kuwa kufanya hivyo ni mwiko mkubwa katika siasa za Tanzania.  Haya yote mbali, lile la kushangaza hasa na kitu ambacho kilikuwa kigeni katika Tanzania ilikuwa yale madai ya kuingiza ubaguzi wa rangi katika siasa za Tanzania. Ilikuwa inastaajabisha kuona magazeti ya TANU yaliyokuwa na sifa ya kuheshima haki za binadamu yakichapisha na kuzipa uzito wa hali ya juu habari za kundi dogo la Waislam waliokuwa wanawalaumu Waislam wenzao wa Kiismailia kwa kutozaliwa weusi. Miaka kumi iliyopita watu wa Tanganyika, Waislam wenyewe waliokuwa ndiyo walioanzisha na kuijenga TANU, walipambana vikali dhidi ya siasa za kibaguzi za Zuberi Mtemvu na chama chake cha African National Congress. Mtemvu alishindwa na matokeo yake ikawa Tanganyika kuwa na serikali ya watu wote isiyobagua rangi na ikitawala raia wa rangi zote kwa misingi ya haki. Kwa ajili hii nchi ikawa haina msuguano kwa ajili ya ubaguzi wa rangi. Haya matokeo mapya yalikuwa hayaendani na misingi ya TANU.
Ilipofikia hali hii, rais wa EAMWS, Tewa Said Tewa na makamo wake Bibi Titi Mohamed, waliamua kulipeleka suala hili kwa Juluis Nyerere, Rais wa Tanzania na mwenyekiti wa TANU, chama tawala. Watu hawa walikuwa wakichekeana jino pembe. Lakini ili tuelewa chanzo cha uadui huu inatulazimu turudi nyuma hadi mwaka wa 1963, katika siku za mwanzo za uhuru, katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU [12]uliofanyika Ukumbi wa Karimjee.
Kama ilivyokwishaelezwa hapo mwanzoni kuwa mwaka 1963 ulikuwa mwaka wa mambo mazito. Ilikuwa ndiyo mwaka ambao Kanisa Katoliki liliteua wagombea wake wapambane na wagombea wa TANU waliokuwa Waislam katika uchaguzi wa serikali za mitaa kule Kigoma na Bukoba. Ulikuwa ndiyo mwaka ambao Rais wa TANU, Nyerere alipombana na EAMWS kupitia Bilali Rehani Waikela. Mwaka wa 1963 ndiyo ulikuwa mwaka ambao Halmashauri Kuu ya TANU ilivunja Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa limetawaliwa na Waislam kwa madai kuwa baraza hilo lilikuwa ‘likichanganya dini na siasa’. Mwaka 1963 ulikuwa mwaka muhimu kwa Halmashauri Kuu ya TANU kwa sababu ilikuwa mwaka ambao ilifanya maamuzi nyeti ya kidini. Mwaka ule Bibi Titi na Nyerere walishambuliana kwa maneno ndani ya Halmashauri Kuu yA TANU kuhusu jambo jingine tena la dini lililokuwa likihusu EAMWS.
Wanakamati wawili wa Halmashauri Kuu ya TANU, Selemani Kitundu na Rajab Diwani, waliiomba Halmashauri Kuu ya TANU imjadili Aga Khan na nafasi yake kama patroni wa EAMWS. Kitundu na Diwani walidai kuwa wana habari Aga Khan anataka kuitawala Tanganyika kupitia Waislam na EAMWS. Kwa ajili hii basi wakapendekeza EAMWS ifungiwe. Nyerere aliwaunga mkono Selemani Kitundu na Rajab Diwani. Bibi Titi akasimama kishujaa dhidi ya Diwani, Kitundu na Nyerere, akasema hakuna kati yao aliyekuwa na haki ya kuifungia jumiaya yoyote ya Waislam. Kama walikuwepo watu ndani ya EAMWS ambao walikuwa wanakwenda kinyume na sheria basi watu hao wapelekwe mahakamani na sheria ichukue mkondo wake. Bibi Titi akaendelea na kusema kuwa EAMWS imekuwepo kabla ya TANU na siku zote imekuwa ikitoa huduma kwa Uislam. Inasemekana hasira zilipanda na kukawa na kutoleana maneno kati ya Bibi Titi na Nyerere. Bibi Titi akamwambia Nyerere yeye hamuogopi yeyote ila Allah.
Tuhuma zile dhidi ya Aga Khan na EAMWS hazikuweza kuthibitishwa na Halmashauri Kuu ya TANU ikaliacha jambo lile kwa wakati ule. Lakini Nyerere alikuwa amefedheheka. Kuanzia hapo akajenga chuki dhidi ya Bibi Titi na kumweka Rajab Diwani na Selemani Kitundu karibu yake. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1965 Bibi Titi na Tewa wakapoteza viti vyao kwa watu ambao walikuwa hata hawafahamiki – A.M. Mtanga na Ramadhani Dollah. Iliaminika kuwa Nyerere alikuwa anahusika na kuanguka kwa Bibi Titi na Tewa. Kuanzia hapo mambo yakawa dhahiri. Nyerere alikuwa amewatangazia vita wote wawili, Bibi Titi na Tewa. Nyerere alikuwa sasa ana imani kuwa wale maadui zake wawili walikuwa wamekwisha kisiasa. Lakini kilichokuwa kkimuudhi Nyerere zaidi ilikuwa taarifa ambazo alikuwa akizipata kuwa Tewa alikuwa akipewa mapokezi makubwa sana na Waislam katika ziara zake huko mikoani  kama rais wa EAMWS. [13]
Sasa mwaka wa 1968, Bibi Titi na Tewa walipokwenda kumuona Nyerere kuhusu jambo lililokuwa linawahusu Waislam, Nyerere alikuwa amejitayarisha vyema. Kiwanuka ameueleza mkutano huu vizuri sana:
…Viongozi hawa wawili wa Waislam walimueleza Mwalimu masikitiko yao jinsi radio ya serikali na magazeti ya TANU yalivyokuwa yakiandika habari kuhusu matatizo yale ya Waislam. Walidai kuwa TANU ilikuwa ikichanganya dini na siasa. Waliokuwa wakimtahadharisha kuhusu jambo hilo hawakuwa wengine ila marafiki zake wa zamani na wa kutumainiwa, Tewa na Bibi Titi. Marafiki wa kutumainiwa kwa sababu ilikuwa Titi aliyemuunga mkono Nyerere katika siku za mwanzo za TANU, pale Suleiman Takadir – mmoja wa wazee wa TANU – aliposema kuwa TANU ilikuwa na Ukristo kama Mwalimu na Rupia, rais na makamo wake walivyokuwa Wakristo.  Yeye mwenyewe akiwa Muislam hasa, aliipatia TANU ushindi kwa kuthibitisha kuwa Tanzania, Tanganyika kama ilivyokuwa ikijulikana wakati ule, ilikuwa mbele, na Uislam unafuata nyuma. Leo, alikuwa anazungumzia jambo ambalo yeye mwenyewe alilishinda katika miaka ya 1950. Jibu walilopata kutoka kwa Mwalimu lilikuwa la kusisimua. Mpashaji wangu habari anasema lilikuwa jibu la mkato. ‘Mmeamua kunipiga vita, jiandaeni.’ [14]
Mwalimu Nyerere alikuwa anawaambia Tewa Said Tewa na Bibi Titi Mohamed uso kwa macho wajiandae kwa kile kilichokuwa dhahiri: vita ya msalaba dhidi ya umoja wa Waislam. Sheikh Suleiman Takadir aliyaona haya na aliiomba TANU toka mwaka wa 1958 pawepo na uhakika kuwa Wakristo ambao walikuwa wanapanda migongo ya Waislam na kuchukua uongozi hawatakuja kuwafanyia uadui Waislam pale Waislam watakapokuwa sasa wanataka kugawana madaraka ya kuongoza nchi sawa na Wakristo baada ya uhuru. Tewa Said Tewa, muasisi wa TANU, waziri katika serikali ya kwanza ya uhuru, balozi katika Jamuhuri ya watu wa China na Rais wa baraza la Tanzania la EAMWS, pamoja na Bibi Titi, mwanamke aliowakusanya wanawake wote nyuma ya Mwalimu Nyerere na TANU, walikuwa wakisemwa na Nyerere kama vile watoto wadogo wa shule waliokuwa watukutu kwa sababu tu, walikuja kumfahamisha Rais kuhusu kukiukwa kwa maadili ambayo ilihitaji yeye ashughulikie mara moja na kutoa uamuzi.
Ulipofika mwezi Oktoba, ‘mgogoro’ ukachukua mwelekeo mpya pale Makamo wa Rais wa Tanzania, Abeid Amani Karume, alipoishambulia EAMWS kuwa ni chombo cha unyonyaji. [15] Kutokea hapo Karume akawa anafanya mashambulizi na kutoa shutuma kwa EAMWS, wakati mwingine akijaribu kufafananisha uhusiano wa EAMWS na Waislam katika mtazamo wa Ki-Marxist, akidai kuwa jumuiya ile kilikuwa ‘chombo cha makabaila wakubwa na kilikuwa chini yao kikiwanyonya watu wa chini’. [16] Mgogoro ulipozidi kukua mashambulizi yakahama sasa kutoka EAMWS na kuhamia kwenye mafunzo ya msingi katika Qur’an Tukufu. Katika mkutano wa hadhara Zanzibar, Karume alitoa changamoto kwa Muislam yeyote ajitokeze bila ya woga kupinga kauli zake mbili kuwa ‘Hakuna tofauti kati ya Uislam na Ukristo’, na ‘Kufunga siyo lazima’.
Lakini juu ya mashambulizi dhidi ya uongozi wa Waislam  kutoka serikalini, Nyerere alikuwa hana uwezo wa kumgusa Mufti Sheikh Hassan bin Amir. [17] Sheikh Hassan bin Amir alikuwa na nguvu sana kiasi cha kwamba si Nyerere au yeyote yule kuweza kumgusa kwa wakati ule. Sheikh Hassan alikuwa kwenye siasa kabla ya vijana waliokuwa katika TANU na nafasi yake katika umma wa Kiislam na uzalendo wake ulikuwa hauna shaka. Sheikh Hassan bin Amir aliingizwa TAA kwa mara ya kwanza mwaka 1950 na Abdulwahid Sykes akiwa mwanakamati katika Kamati ndogo ya siasa ya TAA. Kwa ajili hii basi, akawa mmoja wa wale waliotia sahihi ile memoranda iliyotayarishwa na TAA kwenda kwa Gavana wa Tanganyika, Edward Twining kuhusu mabadiliko ya katiba ya Tanganyika. TANU ilipoasisiwa, Sheikh Hassan bin Amir alikuwa akikiwakatia watu kadi za TANU msikitini huku akidarsisha. Baadhi ya wanachama shupavu wa TANU ambao Sheikh Hassan bin Amir aliwaingiza katika TANU ni Sheikh Mussa Rehani ambae alipewa kadi yake ndani ya msikiti Kigoma. Wakati Nyerere alipokuja TAA Dar es Salaam mwaka 1953, alimkuta Sheikh Hassan bin Amir mwenyeji katika siasa. Baada ya uhuru Sheikh Hassan bin Amir alijiuzulu siasa, kutokana na kauli yake alisema kuwa, ili awatumikie Waislam vyema.
Nyerere alifahamu fika kuwa haitakuwa rahisi kwake kumweka Sheikh Hassan bin Amir kizuizini kama alivyofanya kwa Waislam wengine. Sheikh Hassan bin Amir alikuwa ndiyo Mufti wa Tanganyika na Zanzibar na kwa ajili hii alikuwa na hadhi kubwa katika umma wa Waislam. Halikadhalika haikuwa rahisi kwa yoyote kumkiuka Sheikh Hassan bin Amir na kuchukua uongozi wa Waislam.










[1]Frank Humplink ingawa baba yake ni Mzungu lakini katika mazungumzo yake na mwandishi mara kadhaa bila ya dhamira alijinasibisha na Uchagga kuliko Uzungu. Kwa ajili hii mwandishi ameamua kumtabulisha kamaMchagga.
[2]Mwandishi alipomuhoji Frank Humplink kuhusu nyimbo ile alimfahamisha kuwa serikali iliagiza askari waingie nyumba hadi nyumba kusaka ile santuri na ilipokutwa ilivunjwa.
[3]Angalia Zuhra, 30 Machi, 1955.
[4]Angalia barua katika TNA /57/A. 6/23.
[5]Angalia Maria Nzomo, ‘Kenya: The Women’s Movement and Democratic Change’ in Lernado A. Villon & Philip A. Huxtable, (eds.) The African State at a Critical Juncture: Between Disintegration and Reconfiguration (Lynne & Rienner, Colorado, 1998), uk. 167. Inasadikika kuwa wapo wanawake ambao walishiriki katika harakati za ukombozi wa Kenya katika Mau Mau lakini walioshika madaraka hawataki kuwapa hadhi wanazostahili kama mashujaa wa uhuru. Halikadhalika shujaa kama Dedan Kimathi hajapewa heshima anayostahili kama mzalendo aliyepigania uhuru wa Kenya na akanyongwa na wakoloni wa ajili hiyo. Hadi leo kaburi lake badolipo ndani ya jela aliyonyongewa. Kwa habari zaidi angalia, Willy Mutunga, Constitution Making From The Middle Civil Society and Transition Politics in Kenya, 1992 – 1997, SAREAT, Nairobi, 1999 uk. 1.
 [6] Matawi ya TANU yaliyopigwa marufuku yalikuwa: Korogwe, Handeni, Lushoto na Pangani. Kwa maelezo ya  kina angalia,   Ulotu Abubakar Ulotu, Historia ya TANU, Kilimanjaro Publications, 1980, uk. 77-87.
[7] Nyerere alipokwenda Tabora mwaka 1988  kuadhimisha miaka thelathini ya ‘Uamuzi wa Busara’, Ramadhani Abdallah Singo akiwa mtu mzima wa makamo alimuuliza Nyerere vipi chama kimekuwa mwizi wa fadhila kwa kuwasahau wazalendo waliopogania uhuru wa Tanganyika. Nyerere kuanzia pale kila alipokwenda aliwasifia mashujaa waliopigania uhuru na akaagiza chama iwatafute viongozi waliokiongoza chama kati ya mwaka 1954-1958. Hadi Singo na Kassongo wanafariki hakuna chochote kilichofanyika.
[8] Kuna utata katika kura zilizopigwa. Iliffe, A Modern History... akimnukuu Martin Lowenkopf  ‘Political Parties in Ugandaand Tanganyika’, M.Sc. (Econ.) Thesis, University of London, 1961 amenukuu kura thelathini na saba kuunga mkono kushiriki na ishirini na tatu zilipinga. Abdallah Rashid Sembe alipohojiwa na mwandishi tarehe 6 Julai, 1988 alitoa idadi ya kura kuwa thelathini na mbili ziliunga kushiriki na ishirini dhidi yake. Hassan Issa, ‘Safari ya Tabora’ Taarifa ya mkutano wa mwaka 1958 uliofanyika toka tarehe 21/1/1958 mpaka tarehe 25/1/1958 TANU 51, CCM Archives, anatoa idadi ya kura thelathini na saba kushiriki na kumi na moja dhidi yake. Kwa maelezo zaidi juu ya Mkutano wa Tabora angalia Iliffe, ibid. uk. 556-557.            
[9] Nyerere alizidi kutishika pale mara baada ya maulidi yale yaliyofanikiwa, mwezi Julai, 1968 Tewa akifuatana na masheikh wawili, Athumani Manzi na Sheikh Minshehe Mgumba  akafanya safari ya kutembelea Dodoma, Kongwa, Mpwapwa, Kondoa, Tabora na Kigoma. Huko kote Waislam walikuwa wakijitokezakwa wingi kumpokea kiongozi wao. Tabora ulifanyika mkutano mkubwa uliohutubiwa na Sheikh Jumanne Biasi na Rehani Bilali Waikela. Kigoma Tewa alifanyiwa mapokezi makubwa akasindikizwa na magari hadi Ujiji msafara ukiongozwa na Sheikh Khalfani Kiumbe. Katika ziara hizi Tewa alikuwa akifungua shule zilizokuwa zimejengwa na EAMWS. Ilikuwa Kigoma ndipo Tewa Said Tewa alipoonyeshwa barua kutoka kwa Adam iliyoambatanishwa na miniti za mkutano kati ya Sheikh Abdallah Chaurembo na Sheikh Ramadhani Chaurembo akiuandikia uongozi wa EAMWS Kigoma akiwaomba Waislam wajitoe kutoka EAMWS kwa sababu ilisoma maulidi Ilala. Aliporudi Dar es Salaam Tewa aliufahamisha uongozi wa makao makuu kuhusu barua ile.
[10] Barua ya Mwenyekiti Halmashauri ya Uchunguzi Mogogoro ya Waislam kwa Waziri wa Habari na Utangazaji, 21 Novemba, 1968.
[11] The Nationalist, nukuu kutoka kwa Kiwanuka, uk.81.
[12] Maelezo kutoka mwanakamati wa Halmashauri Kuu ya TANU ambae ameomba jina lake listiriwe.
[13] Mwezi Novemba 1967 Tewa Said Tewa alikuwa amefanya ziara ya Mwanza na  Bukoba iliyokuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa alifanya majadiliano na viongozi wa Waislam wa huko kama Sheikh Amin Abdallah wa Mwanza, Sheikh Ali Migeyo na Sheikh Suedi Kagasheki wa Bukoba.
[14] Kiwanuka, uk.2-3.
[15] Ibid., p.81
[16] The Standard, 9th November 1968 nukuu kutoka Kiwanuka p. 81. Vilevile angalia The Standard, 20 November 1968.
[17] Sheikh Hassan bin Amir alianza kukosana na serekali mara tu baada ya uhuru pale Kanisa Katoliki ilipotoa vitu vya kukumbuka uhuru vilivyokuwa vimenakshiwa na picha za Kikristo. Sheikh Hassan bim Amir alikereka na hili na hasa pale George Kahama, Waziri wa Mambo ya Ndani, alipokwenda Italia kuweka uhusiano baina ya Tanganyika na Vatikano. Kuanzia hapo, Sheikh Hassan bin Amir, kupitia Daawat Islamiyya na kwa kupitia wanafunzi  wake waliokuwa wameenea nchi nzima alianza kuandika khutba za Ijumaa na kuzisambaza katika misikiti ya nchi nzima na khutba hizo zikawa zinasomwa katika sala ya Ijumaa. Ujumbe wake kwa Waislam ulikuwa Waislam watumie fursa iliyoletwa na uhuru kwa kujielimisha ili wagawane madaraka sawa na Wakristo katika kuiendesha nchi. Sheikh Hassan bin Amir akaanzisha mfuko wa elimu ambao Waislam walitakiwa kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule. Kwa ajili ya kuingia kwake kati pale Nyerere alipotaka kuivunja EAMWS, Sheikh Hassan bin Amir akaonekana ni kikwazo kwa Ukristo kuukalia juu Uislam.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment