Home » , , , , » MSAJILI WA VYAMA SIASA AONYA VURUGU ZA WAFUASI WA CHADEMA NA ZITTO

MSAJILI WA VYAMA SIASA AONYA VURUGU ZA WAFUASI WA CHADEMA NA ZITTO

Written By Unknown on Thursday, January 9, 2014 | 8:22 PM

Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujiepusha na vurugu na uvunjifu wa amani kinapotatua mgogoro wake na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe.Mapema wiki hii, wafuasi wa Chadema walipambana na wale wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Zitto katika eneo la Mahakamu Kuu wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa na hatimaye kutolewa hukumu iliyompa ushindi Zitto.Akizungumza kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam, Jaji Mutungi alisema vitendo hivyo vinakiuka sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.“Ninawaasa viongozi wa Chadema na Zitto Kabwe kuwazuia wafuasi wao kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani wa aina yoyote wakati wote ambao mgogoro baina yao unaendelea,” alisema Jaji Mutungi na kuongeza:“Mojawapo ya majukumu ya Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 na kanuni za maadili ya vyama vya siasa ya mwaka 2007 zinazokataza vyama hivyo kuruhusu wanachama au mashabiki wake kujihusisha na vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani.”Amewaasa pia waandishi wa habari kujiepusha kushabikia migogoro hiyo kwani ina athari kubwa katika jamii.“Ni vizuri tukakumbusha kuwa migogoro ndani ya vyama vya siasa ni mojawapo ya vyanzo vya uvunjifu wa amani… ni vizuri waandishi wa habari watafakari kwa undani athari za taarifa zao kwa jamii kabla ya kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mgogoro wa ndani ya chama chochote cha siasa,” alisema Jaji Mutungi na kuongeza:“Napenda pia kusisitiza kwamba ni vyema viongozi na wanachama wa vyama vya siasa waonyeshe ukomavu wa siasa kwa kushughulikia tofauti zao na migogoro baina yao kwa ustaarabu, utulivu na amani huku wakizingatia sheria zote za nchi. Hiyo ndiyo demokrasia ya kweli.” Onyo la Msajili limekuja kutokana na vurugu zilizozuka hivi karibuni baina ya wafuasi wa Chadema na wale wa Zitto wakati wa kesi baina ya pande hizo iliyokuwa inasikilizwa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment